Operesheni ya kuwahamisha watu Aleppo yasitishwa
16 Desemba 2016Awali maelfu ya raia na wapiganaji waasi waliendelea kuhamishwa usiku kucha kutoka mji huo operesheni tete ya uhamishaji iliingia siku ya pili leo
Kwa mujibu wa duru za jeshi la serikali ya Syria pamoja na shirika linalotetea haki za binaadamu la Syria ni kuwa operesheni ya kuwoandoa wakaazi na wapiganaji kutoka mji wa Aleppo imesitishwa leo. Upinzani unaulimiwa kukiuka masharti ya mpango huo ulioanza kutekelezwa jana. Awali shirika la msalaba mwekundu lilisema operesheni ya uhamishaji iliendelea usiku kucha na ingeendelea tena leo mradi kuna watu wanaotaka kuondoka mjini Aleppo. Msemaji wa shirika hilo Ingy Sedky alisema magari ya kuwabeba wagonjwa na mabasi yamekuwa yakiingia na kutoka usiku kucha katika maeneo ya mwisho yaliyodhibitiwa na waasi mashariki mwa Aleppo na maeneo mengine ya mkoa huo.
Awali magari yote yalikuwa katika msafara mmoja, lakini usiku kucha kila basi lilirejea kuwabeba wanaohamishwa punde tu baada ya kuwafikisha waliosafirishwa kwanza.
Kando na mabasi ya kijani ya serikali na magari ya wagonjwa, baadhi ya wakaazi waliondoka kwa kutumia magari yao wenyewe. Ahmed al-Dbis, mkuu wa kitengo cha madaktari wa kujitolea wanaosimamia uhamishaji wa watu waliojeruhiwa amesema watu wote wanawasili katika kituo maalum magharibi mwa mkoa wa Aleppo, na kisha kutoka hapo watakwenda kambini au kujiunga na jamaa na marafiki wanaoishi katika eneo hilo
Amekadiria kuwa karibu watu 6,000 wamehamishwa kutoka Mashariki mwa Aleppo, miongoni mwao watu 250 waliojeruhiwa. Baadhi ya waliowasili wahilitaji matibabu ya dharura na wakahamishiwa Uturuki
Maafisa wa Uturuki wamesema kambi itakayowahifadhi watu wanaohamishwa kutoka Aleppo itajengwa ndani ya Syria karibu na mpaka wa nchi hizo mbili. Kambi hiyo itakuwa na uwezo wa kuwahifadhi watu 80,000. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema nchi yake itaendelea kuwapokea wagonjwa na majeruhi wanaopelekwa nchini humo kutoka Aleppo.
Nilikuwa na mazungumzo na pande tofauti, hasa na rais Putin, kuhusu uhamisho na mchakato wa kusitisha mapigano. Urusi pia ilimuagiza waziri wake wa mambo ya kigeni kushughulikia mchakato huu kwa pamoja. pia nilijadiliana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gueterres na nikamwomba msaada wake wakati wa mazungumzo hayo.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura amesema karibu watu 50,000 bado wamekwama katika mji huo wakiwemo raia 40,000. Mkuu wa jopokazi la kibinaadamu kuhusu Syria linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Jan Egeland amesema mjini Geneva kuwa wengi wa waliohamishwa kutoka Aleppo wataelekea katika ngome ya upinzani ya Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria. De Mistura hata hivyo ameonya kuwa suluhisho la Syria linatajika haraka
Nini kitafanyika Idlib? sahamani kwa kusema hatujui lakini naona kilichotokea Aleppo.na kama hakutakuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano na mazungumzo ya kisiasa, basi Idlib itakuwa Aleppo nyingine
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana baadaye leo kujadili mgogoro wa Aleppo kufuatia ombi la Ufaransa, ambayo inawataka waangalizi wa kimataifa kutumwa katika eneo hilo kufuatilia hali na kuhakikisha kuwa misaada ya kiutu inawafikia walengwa.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya pia walijaribu kuiwekea shinikizo Urusi hapo jana kwa kuitaka iwalinde raia. Lakini Rais wa umoja huo Donald Tusk hata hivyo alikiri kuwa hawana mamlaka ya kuhakikisha kuwa hilo linatekelezwa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel