Operesheni ya NATO dhidi ya Libya itaendelea
15 Aprili 2011Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na marais wa Ufaransa na Marekani, Nicolas Sarkozy na Barack Obama wameapa kuendelea na kampeni hiyo,mpaka azimio la Umoja wa Mataifa litakapotekelezwa. Viongozi hao wametoa tamshi hilo katika hati ya pamoja iliyochapishwa katika magazeti kadhaa.
Marekani yapinga kupeleka ndege kumshambulia Gadaffi
Lakini katika mkutano wa mawaziri wa nje wa jumuiya ya kujihami NATO mjini Berlin, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton, amepinga wito wa Uingereza na Ufaransa kupeleka ndege za kijeshi kushiriki katika operesheni dhidi ya kiongozi wa Libya.
Nae Katibu Mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen, amekariri kuwa operesheni za kijeshi zinapaswa kuendelea ili kuweza kuwalinda raia wa Libya na kupata suluhisho la kisiasa. Wakati huo huo, Gaddafi alizuru mitaa ya mjini Tripoli, muda mfupi tu baada ya mji mkuu huo mkuu wa Libya kushambuliwa na ndege za kijeshi za NATO.