1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni ya uhalifu Kenya yaendelea Bonde la Ufa

23 Februari 2023

Asasi za usalama kutoka eneo la bonde la ufa zimekuwa zikifanya mikutano ya mara kwa mara kuweka mikakati ya usalama, na wametangaza kuwa muda waliopewa majambazi kuwasilisha bunduki haramu kwa hiari umekamilika

Global Ideas Kenia Hirten Laikipia County
Picha: picture-alliance/dpa

Kamishna wa eneo la bonde la ufa Abdi Hassan amesema hapo jana maafisa wa usalama waliweza kutibua njama ya majambazi waliotaka kuwavamia maafisa wa usalama na raia eneo la Kainuk, Turkana.

"Tumekuwa na tukio hapo jana ambapo majambazi hao walijaribu kuwavamia polisi, majeshi na raia lakini walikabiliwa vilivyo. Tulifanikiwa kuwakamata majambazi wawili ambao watafikishwa mahakamani. Kwa ujumla kufikia sasa tumeweza kupokea bunduki 23 zilizosalimishwa na majambazi hao kwa hiari, hususan katika maeneo ya Samburu na Turkana.”

Operesheni hiyo iliyopewa jina "Operation Maliza uhalifu” iling'oa nanga tarehe 15 mwezi huu wa Februari ikiazimia kukomesha uvamizi na mauaji yanayotekelezwa na wezi wa mifugo katika maeneo ya Turkana, Samburu, Pokot magharibi, Elgeyo Marakwet, Baringo na Laikipia.

Kumekuwa na picha pamoja na taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa mitandaoni zikidai kuwa maafisa 11 wa polisi wamewaua kwenye oparesheni hii. 

Viongozi wa eneo la Turkana wakiongozwa na Gavana James Lomurkai wameirai serikali kutumia njia tofauti kuwapokonya majambazi silaha haramu, wakidai mbinu zilizotumika awali zimekuwa na mapendeleo.

Mojawapo wa changamoto zinazotajwa kuchangia hali ya ujambazi usiokuwa na kikomo katika maeneo hayo, ni kwamba kuna silaha zinazopitishwa kwa njia haramu kutoka mataifa Jirani, hasa yanayoshuhudia vurugu. Kamishna Abdi Hassan wa eneo la bonde la ufa anaarifu kuhusu ushirikiano na mataifa Jirani.

Raia wanaoishi kwenye maeneo hao wamehakikishiwa usalama, na wanaeza kuendelea na shughuli zao za kawaida za kila siku.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW