1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni za kijeshi jimboni Tigray kuingia awamu ya mwisho

17 Novemba 2020

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema operesheni za kijeshi jimboni Tigray zitaingia katika awamu ya mwisho, wakati ambapo shinikizo la kimataifa linaongezeka dhidi yake la kuumaliza kwa Amani mzozo huo.

Äthiopien Militärparade in Tigray
Picha: DW/M. Hailesilassie

Hapo jana(16.11.2020) kulifanyika mashambulizi mapya ya anga katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mekele, wakati wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakitoa mwito wa kumalizwa kwa mzozo huo na kufanyika mazungumzo. Hata hivyo Ethiopia imepuuzilia mbali mwito huo. Mmoja wa mashuhuda wa mashambulizi hayo ya anga katika mji mkuu huo wa Tigray, Mekele, anasema:

Abiy, mshindi wa tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel mwaka jana alitangaza kampeni ya kijeshi katika jimbo hilo pinzani mnamo Novemba 4, akisema ilisababishwa na mashambulizi yaliyofanywa na chama tawala cha Tigray, Tigray Peoples Liberation - TPLF kwenye makambi ya kijeshi ya serikali.

Mapigano hayo yamesababisha vifo vya mamia ya raia na wengine 25,000 wakikimbilia nchi jirani ya Sudan, ambako kunatarajiwa wakimbizi wengi huenda wakaingia nchini humo. Mapema leo waziri mkuu Abiy ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba "Muda umekwisha na kufafanua kuwa muda wa siku tatu uliotolewa kwa vikosi maalumu vya Tigray pamoja na wanamgambo ili kujisalimisha kwa vikosi vya serikali badala ya kuendelea kuwa vibaraka wa utawala haramu wa kijeshi umekamilika”.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Minasse Wondimu Hailu/picture alliance/AA

Abiy aliongeza kuwa "Kwa kuwa muda huo umefikia ukomo, katika siku zijazo kutafanyika mashambulizi ya mwisho”,

Kufungwa kwa mawasiliano kumeongeza ugumu wa ufuatiliaji wa mzozo unaoendelea kwenye jimbo hilo. Vikosi vya serikali vinadai kulidhibiti eneo la kaskazini la Tigray kulikokuwa na mapigano makubwa na mwishoni mwa wiki, lilisema walikamata mji wa Alamata uliopo kilomita 180 kusini mwa mji mkuu wa Tigray, Mekele.

Hata hivyo kiongozi wa Tigray Debretsion Gebremichael ameliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali na watu wa Tigray wataendelea kuilinda ardhi yao. Amesema, kampeni hiyo haiwezi kumalizika hadi pale wavamizi watakapotoka kwenye ardhi yao na kuhitimisha akisema hawataweza kuwanyamazisha kwa nguvu ya kijeshi. Debretsion amedai mashambulizi hayo yamewajeruhi raia, ingawa serikali inakataa.Umoja wa Mataifa waonya kuhusu 'uhalifu wa kivita' Tigray

Abiy ameendelea kupuuza miito ya kimataifa ya kuumaliza mzozo huo na kuanzisha majadiliano. Hapo jana, makamu waziri mkuu Demeke Mekonnen alikwenda Uganda na Kenya kukutana na marais wenye ushawishi mkubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliandika kwenye tiwtter baada ya kukutana na kiongozi huyo akisema vita vya Ethiopia vitachafua taswira ya Afrika nzima na kutoa mwito wa mazungumzo. Hata hivyo muda mfupi baadae Museveni aliufuta ujumbe huo na Demeke kuweka wazi kwamba hakuna uwezekano wa mazungumzo hivi karibuni. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya pia alitoa mwito wa suluhu ya amani baada ya mazungumzo na Demeke.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW