Orban kukutana na Zelensky katika ziara yake mjini Kyiv
2 Julai 2024Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban, anatazamiwa hii leo kufanya ziara yake ya kwanza mjini Kyiv tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022. Taarifa hizo zimechapishwa na Gazeti la Financial Times ambalo limenukuu vyanzo vyenye ufahamu na suala hilo na kusema kuwa Orban atakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.
Ziara ya Orban, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa misaada ya kijeshi inayotolewa na nchi za magharibi kwa Ukraine, inafanyika siku moja baada ya Hungary kuchukua urais wa kupokezana wa baraza la Umoja wa Ulaya.
Orban, ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi Vladimir Putin ni miongoni mwa viongozi wa Umoja wa Ulaya, ambaye mara kwa mara amekuwa akipinga mipango mingi ya Umoja wa Ulaya kuunga mkono Ukraine katika kampeni yake dhidi ya uvamizi wa Moscow.