1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Orodha ya wathirika wa mauwaji nchini Burundi yatangazwa

Amida Issa7 Septemba 2021

Tume ya ukweli na maridhiano nchini Burundi, CVR,imetangaza ripoti ya shughuli zake na kwa mara ya kwanza ilifanikiwa kupata orodha za waliouwawa mwaka 1972.

Massenbeerdigung in Gatumba
Picha: picture-alliance/AP Photo

Mabaki ya miili zaidi ya 900 iliyofukuliwa kutoka makaburi ya pamoja, nguo za wahanga wa mauwaji hayo, na vyuma vilivyowekwa juu ya makaburi hayo vilivyotajwa kama vilidhamiria kupoteza ushahidi ndio vilivyooneshwa raia,  viongozi serikalini na waandishi habari waliohudhuria tukio  hilo la kukamilishwa kazi ya tume ya ukweli na maridhiano jijini  Bujumbura.

Mkuu wa tume hiyo, Pierre Claver Ndayicariye, amesema mwaka 1972 watu wengi waliuwawa, baadhi walikuwa maafisa, wengine wafanya kazi wa benki, wanafunzi wa chuo kikuu na wengine waloionekana kutokuwa na kipato.

"Kuna waliouwawa tulioambiwa na familia zao, wengine tulopata orodha, na wengine waliouwawa na miili yao kutupwa katika Ziwa Risizi na Tanganyika. Aprili 1972 wakaazi wa jiji waliona miili zikielea na kulisalia miezi 2, 3 pasina kula samaki waliokuwa wameshiba watu." alisema Ndayicariye.

''Ningewataka kuzingatia ripoti za tume hii''

Tume ya CVR imeahidi kuendesha sensa ya watu wote waliouwawa katika migogoro mbalimbali iliyoisibu Burundi hadi mwaka 2008.Picha: AP/J. Delay

Naibu mkuu wa baraza la seneti, Cyriaque Nshimirimana aliyeiwakilisha serikali amewataka raia kuachana na fikra ya kuwa shughuli za Tume ya CVR ni kufufua chuki za kikabila kati ya wananchi.
"Tumekuwa tukisikia kwamba shughuli za tume hii eti ni za kuja kufufua chuki kati ya raia wa jamii, wengine eti ni tume ya kuja kuwapandisha hawa na kuwashusha wengine. Hii si kweli. Ningewataka kuzingatia ripoti za tume hii.",alisema Nshimirimana.

Baadhi ya raia waliohudhuria tukio hilo la kutangazwa ripoti ya tume CVR wamekaribisha kazi inayoendeshwa na tume hiyo, lakini wamekosoa kuona hadi sasa bado waliopanga mauwaji hayo kutambulika.

Tume hiyo ya ukweli na maridhiano imesema katika majukumu yake ni kuwahamasisha walioendesha mauwaji kuomba radhi na waliofiliwa na ndugu zao kuwapa msamaha.

Tume ya CVR imeahidi kuendesha sensa ya watu wote waliouwawa katika migogoro mbalimbali iliyoisibu Burundi hadi mwaka 2008.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW