Osama aliishi Abbottabad kwa miaka mitano
7 Mei 2011Matangazo
Mke wa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, Osama bin Laden amesema kuwa mumewe ambaye aliuawa katika shambulio la Marekani Jumatatu iliyopita, aliishi na familia yake kwenye eneo lililozungukwa na ukuta huko Abbottabad, Pakistan kwa miaka mitano. Maafisa wa Pakistan wamesema kuwa mke wa bin Laden ambaye ni raia wa Yemen, pamoja na wake zake wengine wawili na watoto wake 13 walikuwa wakipatiwa matibabu pamoja na kuhojiwa. Maafisa wa Marekani wamesema kuwa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda ulikuwa unafikiria kufanya shambulio kwenye treni za Marekani wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001.
Kwa mujibu wa maafisa hao, taarifa hizo ziko kwenye nyaraka zilizopatikana katika maficho ya kiongozi wa al-Qaeda, Osama bin Laden nchini Pakistan. Polisi wa Marekani wanazichunguza nyaraka hizo, kompyuta na DVD zilizokamatwa wakati wa shambulio la Jumatatu ambalo bin Laden aliuawa.
Wakati huo huo, Rais Barack Obama wa Marekani jana Ijumaa alikutana na kuwapongeza wanajeshi wa kikosi maalum cha Marekani ambacho kilishiriki katika operesheni ya mauaji ya bin Laden na kukipongeza kutokana na juhudi zao hizo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFPE)
Mhariri: Mohamed Dahman
Matangazo