Sonko, Mwanasiasa wa upinzani nchini Senegal aachiwa huru
15 Machi 2024Wakili wa Sonko Bamba Cisse ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mteja wake aliyekuwa anazuiliwa gerezani pamoja na mshirika wake mkubwa Bassirou Diomaye Faye wameachiliwa huru.
Faye tayari ameteuliwa kuwa mgombea wa upinzani baada ya Sonko kuzuiwa kuwania nafasi hiyo na haikujulikana mara moja namna hatua hiyo inavyoweza kuwa na athari kwenye uchaguzi huo.
Sonko aliyeshika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa mwaka 2019 anachukuliwa kuwa kitisho kikubwa kwa chama cha Rais Macky Sall, ambaye hagombei tena baada ya maandamano makubwa ya upinzani ya kumpinga na yaliyodumu kwa miezi kadhaa.
Wagombea wa urais nchini Senegal walianza kampeni za uchaguzi siku ya Jumamosi kufuatia wiki za machafuko kote kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya Rais Macky Sall kutangaza kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi.
Soma pia:Wito wa kumwachilia mgombea urais wa Senegal kutoka gerezani
Wanasiasa hawa wameachiliwa muda mfupi baada ya Rais Sall kuiambia serikali yake kuanza mara moja utekelezaji wa sheria ya msamaha mara baada ya kuchapishwa rasmi.
Sall alipendekeza muswada utakaosamehe vitendo vilivyohusika na maandamano ya kisiasa tangu mwaka 2021.