Pakistan katika mzozo zaidi wa kisiasa
26 Agosti 2008Tayari kiongozi wa chama cha Pakistan People Party PPP, ambaye ni mume wa aliyekuwa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo aliyeuawa Benazir Bhutto, Asif Ali Zardari, amewasilisha makaratasi yake ya uteuzi kuwania kiti hicho cha Urais wakati wa uchaguzi utakapoitishwa hapo Septemba 6 mwaka huu.
Chama hicho cha PPP kinapigiwa upato kushinda uchaguzi huo, baada ya kushinda viti vingi bungeni wakati wa uchaguzi mkuu wa mwezi Februari mwaka huu.
Zardari ambaye alichukua hatamu ya uongozi wa chama hicho kufuatia shambulizi la bomu lililomuua mkewe Benazir Bhutto Mwezi Desemba mwaka uliopita, anaamini chama chake cha PPP kitapata ushindi mkubwa wakati wa uchaguzi huo kutokana na kwamba kinaungwa mkono na idadi kubwa zaidi ya wabunge inayohitajika bungeni.
Aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Nawaz Shariff ambaye chama chake kimejitoa katika serikali ya mseto siku ya Jumatatu, kufuatia mzozo wa ndani katika serikali hiyo ya Mseto, kuhusu kurejeshwa nyadhifani kwa majaji walioachishwa kazi, pia amemteua jaji Mstaafu wa mahakama kuu Saeed Uz Zaman Siddiqui kupambana na Zardari.
Uchaguzi huo unafuatia kujiuzulu kwa Rais Pervez Musharraf, kufuatia shinikizo kutoka kwa vyama mseto katika serikali hiyo ya muungano, la kutaka kumshtaki kwa kutumia vibaya mamlaka yake.
Chama cha Pakistan Muslim League ambacho kilimuunga mkono Musharraf, kwa upande wake kimemteua katibu mkuu, Mushahid Hussain, kuwania wadhifa huo.
Wakati huo huo afisa mmoja wa ubalozi wa Marekani nchini Pakistan amenusurika kifo baada ya kufyatuliwa risasi katika eneo la kaskazini magharini mwa Pakistan.
Maafisa wa usalama nchini himo wanasema kuwa Nancy Tracy alishambuliwa kwa bunduki aina ya AK 47 alipokuwa akitoka katika ofisi za ubalozi mdogo wa Marekani Mjini Peshawar.
Aidha katika tukio jingine watu wasiopungua 20 wamejeruhiwa kufuatia mlipuko uliotokea katika jimbo la Baluchistan lenye utajiri mkubwa wa mafuta.Visa vya ghasia vimeongezeka nchini humo huku viongozi wake wa kisiasa wakizozana kisiasa.