Pakistan: Mshambuliaji awaua watu zaidi ya 30 msikitini
30 Januari 2023Shambulizi hilo lilitokea wakati wa ibada ya sala ya alasiri katika mji wa Peshawar karibu na maeneo ya zamani ya kikabila yanayopakana na Afghanistan ambapo idadi ya wanamgambo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku.
Pakistan inashuhudia ongezeko kubwa la mashambulizi ya wanamgambo tangu mwezi Novemba mwaka uliopita, baada ya kundi la Taliban kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano na vikosi vya serikali.
Watu waliouawa wengi wao walikuwa maafisa wa polisi waliokuwa miongoni mwa waumini waliokuwemo kwenye msikiti huo uliopo kwenye kambi ya polisi katika mji huo wa Peshawar, kaskazini magharibi mwa Pakistan.
Katika shambulio hilo la kujitoa muhanga takriban waumini 150 wamejeruhiwa.
Soma pia:Pakistan: Mshambuliaji wa kujitoa muhanga awaua watu zaidi ya 30 waliokuwa msikitini
Polisi wamesema msikiti huo upo ndani ya uwanja ambao pia yapo makao makuu ya polisi ya jiji la Peshawar. Polisi wamesema kati ya waumini 300 hadi 350 walikuwa ndani ya msikiti huo wakati mshambuliaji alipojilipua.
Eneo hilo la polisi liko kwenye sehemuyenye ulinzi mkali pamoja na majengo kadhaa ya serikali, na haieleweki vipi mshambuliaji huyo alivyoweza kupenya na kuingia ndani ya eneo hilo bila kugunduliwa.
Kulingana na afisa wa polisi Zafar Khan, mlipuko huo umeling‘oa paa la msikiti. Afisa mwingine wa polisi aliyenusurika, Meena Gul mwenye umri wa miaka 38, amesema alikuwa ndani ya msikiti wakati bomu lilipolipuka na hajui jinsi alivyonusurika bila kujeruhiwa.
Polisi:Hakuna mtu,kundi kudai kuhusika kwenye shambulio
Afisa mkuu wa polisi katika mji wa Peshawar Saddique Khan amesema mpaka sasa hakuna mtu au kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
Ingawa kundi la Taliban la nchini Pakistan siku zilizopita limekuwa likituhumiwa kuhusika na mashambulizi kama hayo ya kujitoa muhanga.
Eneo la kaskazini-magharibi la Pakistan kwa muda mrefu limekuwa na shughuli nyingi za wanamgambo, ni mahala ambapo serikali kadhaa zinazoingia madarakani zimeshindwa kuweka mamlaka ya sheria.
Kundi la ndani la Taliban linalojulikana kama Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) pia limeota mizizi katika eneo hilo.
Kundi hilo la wanamgambo, la TTP lilianzisha uasi nchini Pakistan katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Linataka utekelezwaji wa sheria za Kiislamu.
Soma pia:Mkuu mpya wa majeshi Pakistan aanza rasmi majukumu yake
Kando na hilo, pia linataka kuachiwa wanachama wake walio kizuizini na kupunguzwa uwepo wa wanajeshi wa Pakistan katika maeneo ya mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitumika kama ngome za kundi hilo.
Baada ya mlipuko wa leo katika msikiti ndani ya eneo la makao makuu ya polisi, serikali ya Pakistan imeiweka nchi katika hali ya tahadhari.