Pakistan: Musharraf abwaga manyanga
19 Agosti 2008Wimbo wa Taifa wa Pakistan:
Hotuba za aliyekuwa rais wa Pakistan , Pervez Musharraf, kwa taifa lake maisha zilianzia kwa wimbo wa taifa. Lakini mara hii, siku ya jumatatu iliopita, hotuba yake haijawa ya kawaida.
"Baada ya kuiangalia hali ilivyo sasa na kuzungumza na washauri wangu, na kwa ajili ya maslaha ya wananchi na nchi, nimeoamua kujiuzulu. Leo nitawasilisha uamuzi wangu huu kwa spika wa bunge."
Punde baada ya kutangaza hivyo jumatatu, sherehe zilisheheni katika miji kadhaa ya Pakistan, watu wakicheza ngoma mabarabarani .
Alisema alichukua hatua hiyo baada ya kuiangalia hali ya mambo na kushauriana na wanasheria pamoja na washirika wake wa kisiasa. Aliyasema hayo uso wake ukionesha ghadhabu.
Alikua hana njia nyingine ila abwage manyanga. Bila ya kufanya hivyo ilikuwa wazi kwamba anakaribisha malumbano na bunge ambalo wanachama wake wengi waliazimia kumuondosha madarakani kutokana na uongozi mbovu na kwenda kinyume na katiba, jambo ambalo lingeitia nchi yake katika mtafaruku ambao matokeo yake hamna mtu aliyeweza kuyatabiri. Hata Marekani, mshirika wa chanda na pete wa mwanajeshi huyo wa zamani, ilijuwa haiwezi kumuokoa. Watawala wa Washington walikua wachaguwe kati ya mambo mawili, ama wamuunge mkono Pervez Musharraf kufa na kupona hadi dakika ya mwisho na kutoujali upinzani wa bunge na wananchi, au wapoteze kabisa imani ya serekali na wananchi wa Pakistan, hivyo kula hasara katika vita vyake dhidi ya ugaidi wa al-Qaida na wa Wataliban katika eneo hilo la dunia. Iliamua kumuacha Musharraf aende na maji, mtu aliyewasiadia kuufukuza utawala mkorofi wa Wataliban nchini Afghanistan.
Lakini alama zilikuwa zimeshachorwa ukutani tangu miezi 18 iliopita. Akizidi kutengwa na hata washirika wake, hasa pale alipomfukuza kazi hakimu mkuu wa nchi hiyo na kufuatiliwa na mashambulio ya miripuko ya mabomu yaliowauwa zaidi ya watu 1,000, akiwemo waziri mkuu wa zamani, Bibi Benazir Bhutto. Mwezi Novemba mwaka jana Musharraf alitangaza sheria ya hali ya hatari ili kulazimisha achaguliwe tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano, kupitia mahakama kuu. Alihoji namna hivi:
"Pakistan iko ukingoni mwa vurugu. Pindi hali hii haitozuwiwa kwa wakati, kutofanya kitu wakati huu, ni kujiuwa kwa Pakistan, na mimi siwezi kuiruhusu nchi hii kujiuwa yenyewe. kwa hivyo, imenilazimu kuchukua hatua hii ili kuhifadhi kipindi cha mpito cha demokrasia ambacho nimekianzisha miaka minane iliopita."
Pigo kubwa lilikua pale washirika wake waliposhindwa vibaya katika uchaguzi wa bunge mwezi Februari mwaka huu. Udhaifu wake ulizidi kuyaumiza masoko ya fedha ya Pakistan. Wawekezaji katika masoko hayo, japokuwa waliiusifu utawala wa Musharraf kwa vile ulikuwa rafiki kwa wawekezaji, sasa yaonesha wamepumua na wamekaribisha kujiuzulu kwa rais huyo. Wanatumai hatua hiyo itamaliza hali ya wasiwasi wa kisiasa iliokuweko.
Serekali ya mseto ilio madarakani imetayarisha mashtaka dhidi ya Musharraf ambayo yanatwama kwamba alikwenda kinyume na katiba na kuiendesha nchi ovyo ovyo. Yeye mwenyewe ameyakanusha madai hayo, lakini alisema nchi itapata hasara pindi atashtakiwa, bila ya kujali matokeo ya mashtaka hayo. Akijipa moyo, alisema hivi katika hotuba yake ya kujiuzulu:
" Ndugu zangu wa kike na wa kiume. Kuondoshwa mimi kwenye uongozi ni haki ya bunge. Na kujitetea ni haki yangu. Hamna karatasi yeyote ambayo inaorodhesha udhaifu dhidi yangu ina haki."
Kwa masiku kumekuweko ripoti kwamba kulikuweko mashauriano ambayo yangepelekea yeye ajiuzulu bila ya kukabiliana na kesi, na hadi sasa haijulikani nini kitakachojiri baadae. Kuna nchi kama vile Marekani, Saudi Arabia na Uengereza ambazo zilijihusisha katika mashauriano baina ya Musharraf na serekali. Maafisa wa serekali walisema Musharraf alitaka apewe kinga ya kutoshtakiwa, lakini katika hotuba yake ya kujiuzulu alisema haombi jambo lolote.
Sababu kubwa ya hatua hii ya Pervez Musharraf ya kusalimu amri inatokana kwa vile yaonesha jeshi la nchi hilo, ambalo yeye alikua analiongoza hadi Novemba mwaka jana, lilimwacha katika mataa. Hivyo, njia nyingine za kukimbilia, kama vile kulivunja bunge au kutangaza sheria ya hali ya hatari, zingeongeza tu shida kwake.
Yeye mwenyewe alisema hataki chochote, tena kwa mtu yeyote, hana hamu ya jambo hilo, na kwamba anauacha mustakbali wake mikononi mwa taifa na wananchi. Katika hotuba yake alijitetea kwa urefu mambo yalivokuwa mazuri wakati wa utawala wake, akisema amerejesha sheria na nidhamu, ameboresha demokrasia na haki za binadamu na kuifanya sura ya Pakistan katika nchi za ngambo in'gare. Kwa jaala ya Mwenyezi Mungu, alisema, Pakistan sasa ni nchi muhimu. Musharraf anahoji aliiongoza nchi kwa nia njema, hasa katika kukabiliana na matatizo ya kiuchumi na kitisho cha siasa za itikadi kali za Kiislamu. Lakini Dr. Christian Wagner wa Wakfu wa Sayansi na Siasa wa hapa Ujerumani ambaye ni bingwa wa masuala ya Pakistan anavoona vingine:
"Nafikiri kwa kujiuzulu Musharraf, vyama vya kidemokrasia katika Pakistan vimepata ushindi muhimu. Nachukulia kwamba pia hali ya usalama itaboreka nchini humo, kwani Musharraf alikua maisha sababu ya malalamiko mengi kwatika miezi iliopita."
Yeye alidai mahasimu wake, wakitenda kwa maslahi yao, walitoa tuhumu za uongo dhidi yake. Kuiweka Pakistan kwanza, alidai , ndio ilikua falsafa yake, na hao maadui wake hawajatambua kwamba wanaweza kufanikiwa kummaliza kisiasa, lakini hawajatambua namna hatua hiyo itakavoipa hasara nchi.
Hapo kabla, Marekani ilisema suala la mustakbali wa Musharraf ni la wananchi wa Pakistan kuamua. Na japokuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, kabla ya kujiuzulu Musharraf, alisema mtu huyo alikua mshirika mzuri wa nchi yake, lakini alikataa kusema kama atapatiwa ukimbizi huko Marekani, jambo hilo kwa sasa halizingatiwi.
Ni mapema mno kuuandika wasifa wa mwisho wa Pervez Musharraf, mtu aliyezaliwa miaka 65 iliopita katika sehemu ambayo sasa iko India, kwani bado yu hai. Katika Pakistan mtu kuondoka au kuondoshwa kutoka wadhifa wa juu wa kisiasa haina maana matu huyo amegeuka kuwa maiti, kisiasa. Mwisho wake hasa ni pale unapotiwa kaburini, na Pervez Musharraf hajafika huko, bado. Ila tu alichelewa kutambua kwamba mchezo umekwisha.