1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Pakistan yaandaa mkutano kujadili kadhia ya Afghanistan

11 Novemba 2021

Pakistan imekuwa mwenyeji wa mazungumzo maalum na wajumbe kutoka Marekani, Urusi na China kujadili juu ya kadhia ya Afghanistan, ambako mzozo mkubwa wa kibinadamu umewalazimisha Waafghani wengi kuikimbia nchi hiyo.

Pakistan | Treffen Vertreter von USA, Russland, China und Pakistan in Islamabad
Picha: Pakistan Ministry of Foreign Affairs/AP Photo/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Taliban Amir Khan Muttaqi pia alikuwepo mjini Islamabad lakini hakuhudhuria mkutano huo maalum uliopewa jina la "Troika Plus.”

Waziri huyo atakutana na waziri mwenzake wa Pakistan baadaye leo. Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Afghanistan Abdul Qahar Balkhi, Muttaqi pia atafanya mkutano na wajumbe maalum kuhusu Afghanistan.

Wajumbe hao maalum wa Marekani, Urusi na China wanatarajiwa kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuitazama Afghanistan kwa jicho la huruma kwa kutoa misaada ya kibinadamu kwa Waafghani. Pia wanatarajiwa kuwahimiza Taliban kuheshimu haki za binadamu na wanawake pamoja na kuhakikisha uwepo wa serikali inayojumuisha pande zote.

Soma pia: UN: Afganistan inakabiliwa na hatari ya janga kubwa la njaa

Haya yanatokea wiki chache tu baada ya Urusi kuandaa mkutano sawa na huu wa leo wa kujadili juu ya kadhia ya nchini Afghanistan, japo wakati huo Marekani haikushiriki.

Jana Jumatano, India ilifanya mkutano na maafisa kutoka Urusi, Iran na maafisa wengine kutoka nchi tano za Asia ya kati kujadili pia juu ya hali ya Afghanistan baada ya Taliban kuchukua usukani wa kuliongoza taifa. Hata hivyo, mkutano huo wa New Delhi ulisusiwa na hasimu wake pamoja na China.

Waafghani wengi wameikimbia nchi hiyo tangu Taliban ilipoingia madarakani 

Waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan Amir Khan Muttaqi(upande wa kulia)Picha: Sergei Bobylev/TASS/dpa/picture alliance

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo, Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi ameonyesha wasiwasi juu ya kuporomoka kwa uchumi wa Afghanistan na athari yake sio tu katika taifa hilo bali katika ukanda mzima wa eneo hilo na sehemu nyengine duniani.

Qureshi amesema, "Tuna imani kuwa mazungumzo haya ya Troika Plus na majadiliano na serikali mpya ya Afghanistan yatasaidia kuleta amani na utulivu, kukuza maendeleo endelevu ya kiuchumi na kusaidia kukabiliana na makundi ya kigaidi yanayoendesha oparesheni zao ndani na nje ya Afghanistan.” 

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Pakistan amesema Afghanistan iko ukingoni mwa kuporomoka kiuchumi, na ameitolea mwito jamii ya kimataifa kuziachilia fedha za nchi hiyo zilizofungiwa ili ziwasaidie Waafghani wenyewe.

Soma pia: Taliban yaahidi ulinzi zaidi misikiti ya Washia

Kundi la Taliban lilichukua madaraka baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini Afghanistan ikihitimisha vita vilivyodumu miaka 20, na tangu kundi hilo lilipoingia madarakani mnamo mwezi Agosti, jamii ya kimataifa haijalitambua kutokana na rekodi yake mbaya juu ya kuheshimu haki za binadamu na ukosefu wa ushirikishwaji kamili kwa jamii yote katika baraza la mawaziri.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW