1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Pakistan yahesabu kura baada ya uchaguzi kumalizika

Sylvia Mwehozi
8 Februari 2024

Pakistan imeanza zoezi la kuhesabu kura baada ya vituo kufungwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika leo na kugubikwa na mashambulizi ya wanamgambo yaliyowaua watu kadhaa na kuzimwa kwa mawasiliano ya simu.

Pakistan | uchaguzi wa bunge
Bango la chama cha Pakistan Muslim League-Nawaz kinachoongozwa waziri mkuu wa zamani wa Nawaz SharifPicha: Navesh Chitrakar/REUTERS

Uchaguzi mkuu katika taifa hilo la Kusini mwa Asia, umefanyika wakati nchi ikikabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na kushamiri kwa ghasia za wanamgambo. Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharifkutoka chama cha Pakistan Muslim League ameelezea matarajio makubwa ya chama chake kushinda uchaguzi wa leo ambao umefanyika katikati mwa vurugu, mvutano mkubwa wa kisiasa na kufungwa kwa mgombea maarufu.

"Maisha ya watu yataboreshwa, Mungu akipenda mfumuko wa bei utakomeshwa na watu wa Pakistan wataishi maisha bora. Hivi ndivyo watu wanavyotamani na ndoto hii inapaswa kutimizwa. Watu hawa waliichafua ndoto hii na kusababisha usumbufu katika jamii yetu, lakini Mungu akipenda tutauponya,”alisema Sharif.

Mabango ya wagombea katika uchaguzi wa Februari 8, 2024Picha: Tanvir Shahzad/DW

Fuatilia ripoti hii: Kwanini Wapakistan hawajali kuhusu uchaguzi ujao

Vituo vya televisheni vinatarajiwa kuanza kutoa mwelekeo wa matokeo ya awali, saa chache baada ya vituo kufungwa. Maelfu ya maafisa wa usalama walikuwa wamesambazwa mitaani na katika vituo vya kupigia kura nchi nzima. Mipaka ya nchi hiyo na Iran na Afghanistan imesalia kufungwa kwa muda wakati vikosi vya usalama vikiimarisha ulinzi.

Wizara ya mambo ya ndani ilisema kuwa hatua ya kuimarisha usalama inatokana nakuuawa kwa watu 26katika mkesha wa uchaguzi kwenye milipuko miwili karibu na ofisi za wagombea kwenye jimbo la kusini magharibi la Balochistan siku ya Jumatano. Baadae kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS lilidai kuhusika na mashambulizi hayo.

Pakistan inakwamaje kuondokana na siasa za matabaka?

This browser does not support the audio element.

Licha ya ulinzi kuimarishwa, ripoti zinasema kwamba watu 9 wakiwemo watoto wawili wameuawa katika milipuko na mashambulizi ya mabomu.

Miongoni mwa waliouawa leo wamo polisi watano waliokufa katika mlipuko wa bomu na kuwafytulia risasi maafisa wa usalama waliokuwa wakipiga doria katika eneo la Kulachi, Kaskazini Magharibi mwa nchi. Watoto wawili walifariki nje ya kituo cha kupiga kura cha wanawake jimboni Balochistan.

Soma pia: Chama cha Khan chatakiwa kutafuta uongozi mpya

Zoezi la upigaji kura limefanyika wakati mamlaka nchini humo zikizima mtandao wa mawasiliano ya simu, hatua ambayo imezusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa viongozi wa vyama vya upinzani. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limeutaja uamuzi huo kuwa ni "shambulizi dhidi ya uhuru wa kujieleza na mkusanyiko wa amani".

Kiasi cha wagombea 18,000 wanawania viti katika bunge la kitaifa na mabunge manne ya kimajimbo huku jumla ya viti 266 vikigombaniwa moja kwa moja na 70 ni kwa ajili ya wanawake na makundi maalumu.

Jumla ya wapiga kura milioni 128 walikuwa wameandikishwa kushiriki uchaguzi wa leo ambao kampeni zake zilifunikwa na kifungo cha waziri mkuu wa zamani Imran Khan.