Pakistan yafanya jaribio la kombora Shaheen II
23 Februari 2007Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la Pakistan kombora hilo lilifanyiwa majaribio katia eneo ambalo halikutajwa lakini lilifanikiwa kufika mahala lilipolengwa.
Jaribio hilo lilishuhudiwa na mwenyekiti wa kamati ya pamoja ya wakuu wa kijeshi wa Pakistan jenerali Ehsan Ul Haq ambae alieleza kuwa mafanikio hayo yanakwenda sambamba na kiu cha Pakistan cha kutaka kufikia usawa na nchi zingine za Asia ya Kusini.
Kombora hilo aina ya Hatf VI au Shaheen II lilifanyiwa majaribio ya kwanza mwezi Machi, mwaka 2005 na kisha katika mwezi Aprili, mwaka uliopita.
Kombora la Hatf VI ndio lenye uwezo mkubwa kabisa katika mpango wa makombora wa Pakistan lenye uwezo wa kufyatuka kwa umbali wa hadi kilomita 2000.
Ni kombora linaloweza kuwekewa miripuko ya nyuklia na ile ya kawaida kwa wakati mmoja.
Taarifa kutoka kwenye makao makuu ya kijeshi nchini Pakistan imesema kuwa jaribio hilo linaambatana na mpango unaoendelea wa kuboresha mfumo wa makombora ya ardhini ya Pakistan.
Jaribio hilo la Pakistan limefanyika siku chache tu baada ya waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Khurshid Mahmoud Kasuri kukupokutana na mwenzake wa India Pranab Mukherjee katika mji wa New Delhi na kutia saini mkataba uliozingatia kupunguzwa athari ya ajali za vita vya nyuklia katika eneo hilo.
Mvutano uliokuwepo awali baina ya Pakistan na India umepungua kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni kufuatia mazungumzo ya amani ya mara kwa mara kati ya pande hizo mbili.
Nchi hizo zinazo miliki nguvu za nyuklia zimejitenga kabisa na mizozo baina yao baada ya kuzuka mvutano wa mwaka 2001 pale India ilipoilaumu Pakistan kwa mashambulio dhidi ya majengo ya bunge mjini New Delhi.
Majeshi ya nchi hizo mbili kwa kawaida yanafahamishana wakati yanapotaka kufanya majaribio ya makombora.
Wachambuzi pia wanasema muda unaotumiwa katika majaribio haya ya makombora baina ya nchi hizi mbili unalingana na sababu za kiufundi na wala sio maswala ya kidiplomasia.