1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan inasema ni lazima Un kuingilia kati

19 Februari 2019

Pakistan imeutaka Umoja wa Mataifa kuingilia kati na kuzima hali ya wasiwasi inayoendelea kupanda baina ya taifa hilo na India kufuatia shambulizi la bomu lililowaua wanajeshi takriban 40 wa India huko Kashmir.

Shah Mahmood Qureshi pakistanischer Außenminister UN Generalversammlung
Picha: Permanent Mission of Pakistan in UN

Waziri wa maswala ya kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureishi amemuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kulishughulikia swala hilo kwa udharura akisema linazidi kuwa tishio kwa usalama kufuatia kauli ya India kwamba itatumia nguvu kuikabili Pakistan inayoituhumu kuhusika na shambulizi hilo.

Katika barua yake kwa Umoja wa Mataifa, Waziri Qureishi alisema kutokana na siasa za ndani, India imeamua kwa makusudi kuzua tena chuki zake dhidi ya Pakistan na hivyo kusababisha mazingira ya hofu na wasiwasi. Kutokana na hilo, ameuambia Umoja wa Mataifa kwamba kuna ulazima kwa wao kuingilia kati kuzima hali ya hofu iliyoko.

Vile vile Pakistan ilimtaka balozi wake nchini India, Suhail Mahmoud, kurudi nyumbani baada ya India pia kumtaka balozi wake wa Islamabad kurudi nyumbani.

Zaidi, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan alisema taifa lake halihusiki kabisa na shambulizi hilo la Kashmir  na kusema Pakistan iko tayari kwa mazungumzo kumaliza hali hiyo tete japo hawatasita kulipiza iwapo India itawashambulia.

Khan alisema India haina ushahidi wowote juu ya madai yake ila wao wako tayari kushirikiana nayo kufanya uchunguzi.

Saudi Arabia kusaidia kutuliza hali baina ya India na Pakistan.

Waziri wa maswala ya kigeni wa Saudi Arabia, Adel Al Jubeir, akizungumza katika mkutano mjini Islamabad, aliahidi kwamba taifa lake litasadia kutuliza hali iliyopo baina ya mataifa hayo mawili ya Asia.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Saudi Arabia Adel bin Ahmed Al-JubeirPicha: Reuters/T. Peter

Mwana wa Mfalme wa Saudia, Mohammad Bin Salman, alifanya mikutano mbali mbali na viongozi wa Pakistan kabla ya ziara yake ya India.

Pakistan na India zimekuwa zikizozania eneo la Kashmir tangu mataifa hayo kupata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1947. Mataifa yote hayo mawili yanadai kumiliki eneo hilo kiasi cha kuingia katika vita mara tatu.

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga alijiripua kwenye msafara wa jeshi la India wiki iliyopita na kuua watu 44. Wanamgambo wa itikadi kali wa kundi la Jaish-e-Mohammed lenye makao yake ndani ya ardhi ya Pakistan walidai kuhusika jambo ambalo limekuwa kiini cha uhasama huo baina ya India na Pakistan.

Mwandishi: Faiz Musa/APE/DPAE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW