1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege ya Pakistan ya msaada wa dawa yawasili Afghanistan

30 Agosti 2021

Wizara ya ulinzi ya Marekani yasema bado kuna kitisho kikubwa cha mashambulio Afghanistan

Eine Maschine der Pakistan International Airlines
Picha: picture-alliance/epa/A. Soomro

Ndege ya Pakistan iliyobeba shehena ya dawa na vifaa vya huduma ya afya imewasili alasiri ya leo ikifikisha mzigo huo kwa mara ya kwanza Afghanistan,tangu ilipoangukia mikononi mwa kundi la Taliban.

Ndege ya Pakistan yenye shehena ya dawa na vifaa vingine vya matibabu iliwasili katika mji wa Kaskazini mwa Afghanistan wa Maza-I Sharif na balozi wa Pakistan mjini Kabul akitangaza kuhusu hatua hiyo ya nchi yake amesema ni sehemu ya kutoa msaada wa kibinadamu wa mahitaji muhimu nchini Afghanistan kwa uratibu wa mashirika ya kimataifa.

Picha: Jafar Khan/AP Photo/picture alliance

Shirika la afya duniani WHO katika taarifa yake limesema ni ndege ya kwanza kati ya tatu za Pakistan zilizopangwa kupeleka msaada wa haraka wa dawa na vifaa tiba katika nchi hiyo inayoshikiliwa hivi sasa na kundi la Taliban. Msaada huo wa  Pakistan unatosha kuwasaidia zaidi ya watu 200,000 wenye matatizo ya kiafya.

Kwa upande mwingine kundi linalojiita dola la kiislamu limedai kuhusika na shambulio la bomu la hivi karibuni huku kundi la Taliban likisema litawashughulikia wanamgambo hao. Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid amesema watakapomaliza kuondoka wanajeshi wa kigeni nchini humo, watayashughulikia mashambulizi yanayopangwa na dola la kiislamu na kutarajia kundi hilo litakomesha mashambulio yao.

Mshambuliaji wa kujitoa muhanga alhamisi wiki iliyopita alishambulia nje ya uwanja wa ndege wa Kabul na kuuwa watu chungunzima wakiwemo wanajeshi 13 wa Marekani waliokuwa wakitarajia kurudi kwao. Marekani ilianzisha mashambulio ya kulipiza kisasi dhidi ya ngome za IS katika siku chache zilizopita hatua ambayo imewaudhi Taliban.

Picha: Fareed Khan/AP Photo/picture alliance

Kundi hilo limesema hawajatoa idhini kuruhusu oparesheni ya aina hiyo na uhuru wa nchi yao unapaswa kuheshimiwa. Kimsingi zoezi la kuwaondoa maelfu ya wageni na waafghanistan walioko hatarini chini ya utawala wa Taliban linatarajiwa kukamilika kesho Jumanne ikiwa ni pamoja na kukamilika hatua ya kuondoka kabisa wanajeshi wote wa Marekani na Jumuiya ya kujihami ya Nato.

Lakini wakati huohuo mjini Brussels Umoja wa Ulaya unajitahidi kuzuia kuwaachia wakimbizi kutoka Afghanistan kuingia katika nchi za Umoja huo bila ya kudhibitiwa. Hayo yamebainika kwenye taarifa iliyoandaliwa kutangazwa katika mkutano maalum utakaofanyika Jumanne, kuhusu Afghanistan. Umoja wa Ulaya umepania kuepusha marudio ya kile kilichotokea mwaka 2015 ambapo wimbi kubwa la kumiminika wakimbizi na wahamiaji lilishuhudiwa katika nchi za Jumuiya hiyo ambazo zilikuwa hazijajipanga na kuzusha mgawanyiko mkubwa miongoni mwao, hali ambayo vile vile ilisababisha kuwapa nguvu vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia katika nchi kama Ugiriki, Italy na kwengineko.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW