Pakistan yasema imeshambulia vituo vya kijeshi Afghanistan
15 Machi 2026
Mvutano wa kijeshi unaendelea kati ya Pakistan na Afghanistan baada ya Islamabad kusema kuwa jeshi lake limefanya mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi na maficho ya wanamgambo kusini mwa Afghanistan.
Kwa mujibu wa vyanzo vya usalama, mashambulizi hayo yalilenga miundombinu ya kijeshi na ghala la vifaa katika mji wa Kandahar, ambao pia ni ngome ya kiongozi mkuu wa Taliban, Hibatullah Akhundzada. Shambulio lingine liliripotiwa kulenga handaki linalodaiwa kutumiwa na wapiganaji wa Taliban na kundi la TTP.
Wakaazi wa Kandahar wamesema waliona ndege za kijeshi angani na kusikia milipuko usiku. Serikali ya Taliban kupitia msemaji wake Zabihullah Mujahid imesema mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mdogo katika kituo cha kuwasaidia waraibu wa dawa.
Mapigano katika mpaka wa nchi hizo yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, huku Umoja wa Mataifa ukisema takribani raia 75 wameuawa na zaidi ya 190 kujeruhiwa tangu mwishoni mwa Februari.