Pakistan yataka Iran ishirikishwe suluhisho la Yemen
7 Aprili 2015Badala yake Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif, alikiambia kikao maalum cha bunge kilichoitishwa kujadili hatua ya nchi yake kujiunga na kampeni hiyo nchini Yemen, kwamba jitihada za kidiplomasia zinazoongozwa na Uturuki na Iran zinapaswa kupewa nafasi na kwamba huenda zikazaa matunda hivi karibuni.
Awali Saudi Arabia ilikuwa imemuomba mshirika wake huyo wa siku nyingi kuchangia ndege za kijeshi, meli na wanajeshi wa ardhini kwenye operesheni ya kuwang'oa waasi wa jamii ya Houthi ambao wanafuata moja ya matapo ya madhehebu ya Kishia nchini Yemen, na ambao wanadaiwa kuungwa mkono na Iran.
Hata hivyo, Sharif alisema hatua kama hiyo ilikuwa inahitaji ridhaa ya bunge, na hadi sasa hakuna mbunge aliyeiunga mkono. Badala yake, Sharif naye amegeukia upande zaidi wa diplomasia.
"Iran inapaswa pia kufikiria sera yake kuelekea Yemen na kujitathmini ikiwa sera hiyo ni sahihi au la. Leo Rais Tayyip Erdogan anafanya mazungumzo na Rais wa Iran. Ninatarajia kwamba kufikia kesho atakuwa amerejea kwetu kutueleza yaliyoafikiwa", alisema waziri mkuu huyo bungeni siku ya Jumanne (Aprili 7).
Sharif, ambaye mwenyewe alihifadhiwa na Saudi Arabia baada ya kupinduliwa na jeshi mwaka 1999, aliwataka wabunge kujadili kwa makini suala hilo bila haraka, akisema hataki kuwarubuni ili wampe idhini.
Diplomasia ya Iran, Uturuki na Pakistan?
Mazungumzo zaidi yanayozijumuisha Iran, Uturuki na Pakistan yanatazamiwa hivi karibuni, baada ya Sharif kukutana na mwenzake wa Uturuki, Ahmet Davutoglu mjini Ankara hapo Ijumaa, ambapo wote wawili walisisitiza kupatikana suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Yemen. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, atawasili nchini Pakistan kesho kujadiliana suala hilo hilo.
Hapo jana, meli ya kivita ya Pakistan iliwaokoa raia wengine 146 wa nchi hiyo waliokuwako Yemen sambamba na raia 36 wa nchi nyengine.
Katika suala hili la Yemen, Pakistan inajikuta kwenye njiapanda. Kwa upande mmoja, imekuwa mshirika wa muda mrefu wa kijeshi na Saudi Arabia ambayo pia inafaidika nayo kwa kununua mafuta kwa bei ya chini. Lakini kwa upande mwengine, inachangiana mpaka mrefu na Iran upande wake wa magharibi, ikiwa pia na mgogoro wa Shia na Sunni ndani yake yenyewe.
Hayo yakiripotiwa, kwenyewe Yemen wapiganaji wa kundi la al-Qaida wamekivamia kituo cha mpakani mwa Saudi Arabia na kuwauwa wanajeshi wawili. Washambuliaji hao wamechukuwa udhibiti wa kituo hicho kilicho umbali wa kilomita 440 kutoka mji mkuu, Sana'a.
Wakati huo huo, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema ndege yake ya kwanza iliyobeba chakula na madawa imewasili mjini Sana'a, kufuatia makubaliano kati yake na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na waasi wa Houthi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Oummilkher Hamidou