1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakanusha makubaliano mapya na Marekani

13 Agosti 2026

Watu wanaofahamu mazungumzo hayo wameliambia shirika la habari la dpa kwamba mkataba huo unaweza kurefushwa kwa hadi siku 60 au hata 90 zaidi. Ingawa haijaamuliwa kama makubaliano hayo yatatangazwa hadharani.

2026 I Hormuz
Mlango bahari wa HormuzPicha: Fatima Shbair/AP Photo/picture alliance

 Pakistan ambayo imekuwa inaongoza juhudi za upatanishi katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran imesema mkataba wa amani kati ya Marekani na Iran utarefushwa ila chanzo kikuu kutoka Iran kinasema nchi hiyo na Marekani bado zinasalia njia panda kuhusiana na kurefushwa kwa mkataba huo.

Watu wanaofahamu mazungumzo hayo wameliambia shirika la habari la dpa kwamba mkataba huo unaweza kurefushwa kwa hadi siku 60 au hata 90 zaidi. Ingawa hata hivyo wamesema bado haijaamuliwa kama makubaliano hayo mapya ya kusitisha mapigano yatatangazwa hadharani.

Taarifa hiyo inakuja saa chache kabla ya kumalizika kwa muda wa siku 60 za mazungumzo zilizowekwa awali kwa ajili ya makubaliano ya kati ya Marekani na Iran.

Waziri mkuu wa Pakistan Shehbaz SharifPicha: Pakistan Prime Minister Office/Handout/AFP

Katikati mwa mwezi Juni, Marekani na Iranzilikubaliana, kupitia mpatanishi wao Pakistani, kuhusu makubaliano ya mpango huo ambao ulitoa nafasi ya kusitisha mapigano na uliokusudiwa kuandaa njia ya kukomesha vita kupitia mazungumzo kwa kipindi cha miezi miwili.

Mashambulizi ya pande zote mbili

Hata hivyo, kumekuwa na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa pande zote mbili, hasa katika nusu ya pili ya mwezi Julai, na matokeo yake, hakuna mazungumzo ya kina yaliyofanyika.

Huko Iran kwenyewe, chanzo kikuu kimesema hakukuwa na maendeleo katika mazungumzo hayo ya kurefusha mpango huo wa mpito uliokubaliwa mwezi Juni.

Maoni hayo yanakuja huku Rais wa Marekani Donald Trump akitoa kauli za kuukebehi utawala wa Tehran na kuendelea kufifisha zaidi matumaini ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Aaron Schwartz/ABACAPRESS/IMAGO

Marekani inaishutumu Iran kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya kufungua tena njia muhimu ya meli katika Mlango Bahari wa Hormuz huku Iran nayo ikiituhumu Marekani kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuondoa vizuizi katika bandari za Iran, kuviondoa vikwazo na kuachilia mali za Iran zinazozuiliwa.

Kwa hivyo licha ya kuwepo kwa taarifa hiyo ya uwezekano wa kurefushwa kwa mkataba wa amani kati ya Iran na Marekani bado nchi hizo zinasalia katika mvutano kuhusu kufikia makubaliano ya kuvimaliza vita huko mashariki ya kati. 

Makubaliano ya hivi punde yanayoendelea ni kati ya Iran na Oman kuhusu usafirishaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz ambayo yanaelezwa kufikia katika hatua nzuri. Vyanzo vya usalama vya Pakistan vinasema makubaliano baina ya pande hizo mbili yanaweza kufikiwa kabla ya siku ya Jumamosi.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW