Rais wa Palestina ataka kuitishwa mkutano mkuu
21 Februari 2018Abbas pia ameondoa uwezekano wa Marekani kuwa mpatanishi katika mzozo wake na Israel.
Katika hotuba yake ya kwanza kwenye baraza hilo tangu mwaka 2009 rais huyo ametaka kuandaliwe mkutano wa kimataifa wa amani utakaohudhuriwa na mataifa mbali mbali ifikiapo katikati ya mwaka huu wa 2018 na lifuatie suala la kukubaliwa kwa Palestina kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Baraza Kuu la Umoja la Umoja wa Mataifa liliitambua Palestina kama mwanachama muangalizi katika baraza hilo mwaka 2012 licha ya Marekani kupinga. Palestina na Vatican ndio wenye hadhi ya wanachama waangalizi pekee katika Baraza Kuu.
Abbas amekanusha kwamba Palestina ilikataa fursa ya mazungumzo
Marekani na washirika wake walizuia jaribio la awali la Abbas kupata uanachama kamili wa Palestina mwaka 2011. Abbas pia ameelezea kutoridhishwa kwake na hatua ya Marekani mwezi Desemba kuitambua Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel na mpango wake wa kuuondoa ubalozi wake kutoka Tel Aviv akisema mpango huo unastahili kubadilishwa ili utoe nafasi ya suluhu la mataifa mawili.
Rais huyo pia amekanusha madai kwamba upande wake ulikataa fursa ya mazungumzo ya kutafuta amani kwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Danon amemtuhumu Abbas kwa kutokuwa mkweli akisema kiongozi huyo wa Palestina alikataa kukutana hata mara moja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati alipofanya ziara saba katika Umoja wa Mataifa.
"Hatujawahi kukataa mwaliko wowote wa kushiriki majadiliano. Tafadhali usiseme kwamba tumekataa mazungumzo," alisema Abbas. "Tunaamini kwamba majadiliano ndiyo njia ya pekee ya kupata amani. Kwa hiyo tuyakatae mazungumzo kivipi, kwa hiyo amini huu sio ukweli," aliongeza Rais huyo wa Palestina.
Antonio Guterres asema hakuna njia nyengine ya suluhu la mataifa mawili
Abbas alizungumza wakati ambapo wajumbe wawili kutoka katika serikali ya Trump kuhusu mchakato wa amani juu ya mzozo huo wa Mashariki ya Kati Jared Kushner na Jason Greenblatt walikuwa wamekaa katika Baraza hilo la Usalama wakimsikiliza.
Lakini aliondoka bila ya kuzungumza nao au hata kumsikiliza Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley akisema marekani iko tayari kufanya kazi na utawala wa palestina.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza kwamba hakuna njia nyengine katika kutafuta suluhisho la kupatikana mataifa mawili kwenye mzozo huo. Amepinga suala la suluhu la taifa moja akisema haiwezekani kutokana na masuala ya haki ya kitaifa, kihistoria na kidemokrasia waliyo nayo Waisraeli na Wapalestina.
Mwandishi: Jacob Safari/APE/DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu