Palestina kuwasilisha ombi la kujiunga ICC
2 Januari 2015Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliitolea wito ICC kulikataa ombi la Palestina kujiunga na mahakama hiyo, aliloliita la kinafiki. Kwa mujibu wa Netanyahu, serikali ya Mamlaka ya Palestina si dola, bali kundi lililounda ushirikiano na kundi jengine la kigaidi, Hamas, ambalo linafanya uhalifu wa kivita.
"Israel ni dola linalofuata sheria na lenye jeshi lenye maadili linaloheshimu sheria zote za kimataifa. Tutawalinda wanajeshi wetu kama wao wanavyotulinda sisi." Ilisema taarifa iliyotolewa na ofisi ya Netanyahu, baada ya kikao cha dharura kwenye makao makuu ya wizara ya ulinzi hapo Alhamisi.
Siku ya umatano, Rais Abbas alisaini mkataba wa ICC na makubaliano mengine 19 ya kimataifa, kufuatia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku moja nyuma, kulikataa pendekezo la Palestina kuitaka Israel ikomeshe ukaliaji wake kufikia mwaka 2017.
"Tunataka kulalamika. Israel inatushambulia sisi na ardhi yetu kila siku. Sasa tulalamike kwa nani, ikiwa Baraza la Usalama limetuangusha?" Abbas aliuambia umma wa waandamanaji mjini Ramallah hapo juzi, baada ya mkutano wa dharura na serikali yake.
Marekani, Israel zakasirika
Marekani na Israel zilichukizwa sana na hatua ya Abbas kusaini mkataba huo, ambapo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Jeffrey Rathke, alisema ni hatua isiyo na manufaa kabisa, na ambayo haipiganii matakwa ya Wapalestina ya kuwa na dola huru yenye mamlaka kamili.
Kwa mujibu wa kanuni za ICC, uwanachama wa Palestina utairuhusu mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, kuchunguza tuhuma za uhalifu wa kivita uliotendwa ndani ya ardhi ya Palestina, bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambako Israel inakingiwa kifua na Marekani.
Ingawa Israel si mwanachama wa mahakama hiyo, raia wake wanaweza kushitakiwa kwa matendo yao katika ardhi ya Wapalestina.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba