Palestina yaidhinishwa kuwa mjumbe asiyekuwa dola UN
30 Novemba 2012Palestina imepewa hadhi ya kuwa mwanachama asiyekuwa dola katika Umoja wa Mataifa baada ya kupata kura za ndio 138 hapo jana za nchi wanachama wa Hadhara Kuu ya Umoja huo kati ya wanachama wote 193 wa baraza hilo.
Nchi tisa zikiongozwa na Marekani na Israeli, zimepiga kura ya kulipinga azimio hilo, huku nchi 41 zikiwa hazijapiga kura kabisa, ikiwemo Ujerumani na Uingereza.
Akizungumza baada ya kura hiyo kupigwa mjini New York, Rais wa Palestina, Mahmud Abbas amesema ushindi huo wa kihistoria ni hatua moja mbele kuelekea uhuru wa nchi yake.
Amesema Wapalestina bado wana safari ndefu katika kujipatia dola kamili na kutoa wito wa kumalizika kwa mgawanyiko uliopo baina ya kundi pinzani la Hamas linaloudhibiti Ukanda wa Gaza.
Marekani na Israeli yakosoa hatua ya UN
Ushindi huo wa Palestina umeonyesha kushindwa kidiplomasia kwa Marekani na Israeli ambazo ziliungwa mkono na mataifa machache kupinga hatua ya kuipandisha hadhi Palestina kuwa kama mwangalizi kwenye Umoja wa Mataifa kama ilivyo kwa Vatican.
Nchi hizo mbili zimepinga azimio hilo zikisema kuwa itakuwa kikwazo katika kutafuta amani ya kudumu ya Mashariki ya Kati. Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, amelaani vikali hatua hiyo kwa kile alichokiita hotuba ya sumu kutoka kwa kiongozi huyo wa Palestina ambaye ameishutumu Israeli kutokana na propaganda za uongo.
Israeli imesema njia pekee ya kupatikana kwa amani ni kufikiwa kwa makubaliano baina ya Israeli na Palestina na siyo kwa njia ya maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton amekosoa hatua ya Palestina kutambuliwa na Umoja wa Mataifa akisema itakuwa kikwazo kwa amani kati ya Wapalestina na Waisraeli.
Marekani imesema azimio hilo limepitishwa kwa bahati mbaya na halina manufaa na kwamba linaongeza vikwazo zaidi kuelekea kwenye mpango wa amani, ndiyo maana nchi yake imelipinga.
Ramallah washangilia ushindi
Ushindi huo umepongezwa na baadhi ya mataifa, ikiwemo Vatican. Katika mji wa Ramallah, kwenye Ukingo wa Magharibi, watu wamejitokeza mitaani kushangilia ushindi huo wa kihistoria. Wananchi hao walikuwa wakipeperusha bendera za Palestina na kupiga honi barabarani huku wakisema "Mungu ni Mkubwa".
Baada ya ushindi huo wito sasa umetolewa wa kuendelea kwa mchakato wa mazungumzo ya amani kati ya Israeli na Palestina.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE
Mhariri: Yusuf Saumu