1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yaandaa rasimu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Deo Kaji Makomba
24 Februari 2020

Umoja wa mataifa jumatatu hii, umesema kuwa, pande zinazohasimiana nchini Libya zimeandaa rasimu ya makubaliano ya kusitisha mapigano wakati wa mazungumzo ya kijeshi yaliyofanyika mjini Geneva.

LNA Chef Khalifa Haftar
Picha: picture-alliance/ Balkis Press

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imesema kuwa matokeo ya mazungumzo hayo yaliyomalizika Jumapili iliyopita, yalikuwa na lengo la kuwarudisha salama wakaazi katika maeneo yao.

Rasimu hiyo ya makubaliano itawasilishwa kwa wa Libya katika serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya GNA na kiongozi wa jeshi la waasi, General Khalifa Haftar kabla ya mazungumo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuendelea mwezi Machi mwaka huu.

Wakati huo huo, mazungumzo ya kisiasa yamepangwa kuanza chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano huko mjini Geneva.

Ingawa Waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa, GNA, Mohamed Taha Siala, Jumatatu hii amesema kuwa, ratiba inaweza isiende kama ilivyopangwa kufuatia mpatanishi wa Umoja wa Mataifa, Ghassan Salame kutokutoa mwaliko rasmi kwa pande zote.

Wanajeshi watiifu kwa mbabe wa kivita nchini Libya Khalifa Haftar.Picha: AFP

Siala pamoja na waziri mkuu wa serikali ya Libya Fayez serraj, walikuwa mjini Geneva kuhudhuria mkutano wa Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Kwenye hotuba yake mbele ya chombo cha juu cha haki cha Umoja wa Mataifa, Serraj alimshutumu Haftar kuwa ni mhalifu wa kivita huku akisisitiza kuwa kila wakati serikali yake imeonyesha utayari wake wa kusonga mbele kwenye njia ya amani na utulivu.

Jumamosi iliyopita baraza la ushauri la serikali liliongeza mashariti mengine ili kushiriki katika mazungumzo hayo ya kisiasa.

Baraza kuu mjini Tripol, lilidai maendeleo katika mazungumzo ya kijeshi, orodha ya wajumbe wa upande mwingine na pia utaratibu ulio wazi wa mazungumzo.

Mazungumzo ya kuweka silaha chini nchini Libya, yalifanyika mwezi Januari mwaka huu chini ya mataifa ya Urusi na Uturuki mataifa yanayounga mkono pande zinazohasimiana nchini humo.

Katika mazungumzo ya mjini Berlin mnamo mwezi Januari, viongozi wa kimataifa walikubaliana juu ya mchakato wa amani nchini Libya utakaohusisha jeshi, siasa na namna ya kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW