1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu Libya zasaini makubaliano kusitisha vita

23 Oktoba 2020

Pande zinazohasimiana nchini Libya zimesaini makubaliano ya kudumu ya kusitisha vita. Umoja wa Mataifa umesifia na kupongeza maafikiano hayo. Umoja wa Mataifa umetaka pia kuondolewa mamluki wote nchini Libya.

Kombobild | Schweiz Genf | Gespräche zu Waffenstillstand in Libyen - A. Amhimmid Mohamed Alamami und Ahmed Ali Abushahma
Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Kaimu mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams, amesema makubaliano hayo ya kusitisha vita yataanza kutekelezwa mara moja.

Amesema kulingana na mkataba huo, wapiganaji wote wa kigeni wanapaswa kuondoka Libya katika kipindi cha miezi mitatu, na kikosi kipya cha pamoja cha polisi ndicho kitakachoshika doria katika maeneo yanayozozaniwa.

Williams alizipongeza pande zote mbili husika kwa makubaliano hayo ambayo kwa mara ya kwanza kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, yamewezesha ndege ya abiria kupaa kutoka mji wa Tripoli na kutua katika mji wa Benghazi, mashariki mwa nchi hiyo.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams.Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Uhasama kati ya serikali ya GNA na upande wa Khalifa Haftar LNA


”Safari imekuwa ndefu na ngumu. Uzalendo wenu ndio ulikuwa mwongozo wenu na mliweza kuafikiana kusitisha vita.” Alisema Williams baada ya makubaliano hayo kusainiwa.

Soma pia: UN yahimiza pande hasimu Libya kutanguliza maslahi ya nchi

Mazungumzo hayo ya hivi karibuni yalijiri baada ya serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa kimataifa, kuvishambulia vikosi vya jenerali wa kivita Khalifa Haftar vyenye makao yao mashariki mwa Libya mnano mwezi Juni, kuyajibu mashambulizi yao ya miezi 14 dhidi ya mji mkuu Tripoli.

Tangu wakati huo, makabiliano yametulia magharibi na katikati mwa mji wa bandari wa Sirte, na vikosi vya mashariki pia vimeondoa vikwazo dhidi ya usafirishaji wa bidhaa za mafuta. Vikwazo hivyo vilivyodumu kwa miezi minane viliathiri hali ya fedha kwa taifa na pia kwa pande zote.

Makubaliano mapaya yahitajika

Hata hivyo ipo haja ya kufanyika makubaliano mapana kati ya makundi yenye silaha pamoja na nchi washirika kwenye machafuko hayo, ili mgogoro huo ambao umedumu kwa miaka mingi na kusababisha umwagikaji damu umalizike kabisa.

Waziri mkuu wa serikali inayotambuliwa kimataifa, Fayez al-sarraj.Picha: Media Office of the Prime Minister/Handout/Reuters

Mazungumzo ya kisiasa kati ya pande hizo mbili ambazo hujumuisha miungano isiyo imara lakini yenye masilahi ya ndani, yanatarajiwa kufanyika mapema mwezi ujao nchini Tunisia.

Soma pia: Libya: Mkuu wa serikali inayotambuliwa na UN kujiuzulu

Hata hivyo, juhudi za awali za kidiplomasia kusuluhisha mzozo wa Libya hazikufaulu, kutokana na mvutano ambao umekuwepo kati ya makundi mbalimbali tangu mwaka 2011 wakati aliyekuwa rais wa nchi hiyo Muammar Gaddafi alipoondolewa madarakani.

Wasiwasi wa kuwepo suluhisho la kudumu kisiasa

Tarek Megerisi ambaye ni mchambuzi wa masuala ya sera ya mpango wa Afrika kaskazini na Mashariki ya Kati katika Baraza la Ulaya kuhusu mahusiano ya nje, amesema ni muendelezo mzuri wa mafanikio, matumaini na maelewano.

Lakini bado hakuna ishara ya wazi kwamba, pande zonazozozana Libya haziangalii hatua hii kama kitu kingine bali kama kipindi tu cha kujiandaa na kuweka nafasi ya kuweza kutawala awamu inayofuata ya siasa za mpito nchini Libya.

Soma pia: Vikosi vya Haftar vyalipuuza pendekezo la GNA
 

Huku machafuko ya Libya yakiyavutia mataifa ya nje kwa manufaa ya masilahi yao wenyewe, pande zote zimepata msaada wa silaha na wapiganaji kutoka mataifa ya nje.

Wapiganaji wa kigeni watakiwa kuondoka Libya

Serikali inayotambuliwa kimataifa inaungwa mkono na Uturuki, huku nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu, Urusi na Misri zikiunga mkono vikosi vya Khalifa Haftar.

Umoja wa Mataifa umezihimiza nchi za kigeni kwenye machafuko hayo, kukoma kuingilia masuala ya Libya huku ukizikosoa kwa kukiuka marufuku ya silaha.

(APE,AFPE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW