1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Pande hasimu zaheshimu usitishaji mapigano Sudan

19 Juni 2023

Hali ya utulivu imeshuhudiwa nchini Sudan wakati pande zinazopigana zikijaribu kwa mara nyingine kusitisha makabiliano baada ya miezi miwili ya mapambano makali.

Utekelezaji wa kusitisha mapigano waheshimiwa Sudan
Utekelezaji wa kusitisha mapigano waheshimiwa SudanPicha: AP/dpa/picture alliance

Wakaazi wa mji mkuu Khartoum na mji pacha wa Omdurman wamearifu juu ya kuwepo hali ya utulivu kwenye saa za mwanzo za utelekezaji makubaliano mapya ya kusitisha vita yaliyoanza kufanya kazi asubuhi ya jana Jumapili.

Usitishaji huo mapigano wa siku tatu uliafikiwa siku ya Jumamosi chini ya juhudi za upatanishi za Marekani na Saudi Arabia.

Mataifa hayo mawili kwa pamoja yamekuwa yakiongoza jitihada za kidiplomasia za kumaliza vita nchini Sudan ambavyo tayari vimesababisha vifo vya mamia ya watu na mamilioni wengine wameikimbia nchi hiyo.

Kwenye taarifa yao ya pamoja Marekani na Saudia zilisema pande mbili hasimu nchini humo yaani jeshi la taifa linaloongozwa na Jenerali Abdul-Fattah al Burhan na kikosi cha mgambo wenye nguvu cha RSF chini ya Jenerali Mohammed Hamdani Dagalo zimeafiki kujizuia kushambuliana ndani ya muda wote wa usitishaji mapigano.

Makubaliano hayo ya sasa ni ya hivi karibuni kabisa baada ya yale yaliyotangulia kushindwa kuheshimiwa na kila upande kuulaumu mwingine kwa kuyavunja.

Umoja wa Mataifa waitisha mkutano wa kuchangia fedha za msaada wa kiutu 

Vita vimefanya uharibifu mkubwa nchini Sudan Picha: Satellite image ©2023 Maxar Technologies/AFP

Utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano umeanza siku moja kabla ya mkutano wa kimataifa wa kuchangisha fedha za kugharamia mahitaji ya msaada wa kiutu nchini Sudan.

Mkutano huo unaofanyika leo Jumatatu umeandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na nchi nyingine kadhaa duniani. Umoja huo unasema unahitaji kiasi dola bilioni 2 kufadhili shughuli zote za kiutu nchini Sudan mwaka huu.

Mbali ya kiwango hicho, Umoja wa Mataifa unahitaji vilevile dola nyingine milioni 470 kusaidia mzozo wa wakimbizi kwenye eneo la pembe ya Afrika.

Majarani wa Sudan nao wanahitaji msaada baada ya kuwapokea mamia kwa maelfu ya raia wa nchi hiyo waliokimbia vita.

Umoja wa Ulaya waipatia Misri mchango wa kuwasaidia wakimbizi wa Sudan

Mataifa jirani na Sudan ikiwemo Chad na Misri yamepokea maelfu ya wakimbizi wa nchi hiyo.Picha: Blaise Dariustone/DW

Misri ni miongoni mwa mataifa jirani na Sudan yaliyopokea wakimbizi wa nchi hiyo. Kupitia mpaka wake wa kusini, Misiri imewapokea wakimbizi wengi wakati yenyewe inaandamwa na upungufu mkubwa wa fedha.

Hapo jana Umoja wa Ulaya ulitangaza kuipatia nchi hiyo euro milioni 20 kuipiga jeki katika kuwashughulikia wakimbizi. Msaada huo ulitangazwa na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Jossep Borell aliyekuwa ziarani mjini Cairo 

"Ndani ya siku chache, zaidi ya watu 200,000 wamepokelewa na Misri, inafaa niwashukuru sana kwa kufanya hivo na pia Umoja wa Ulaya utatoa msaada wa haraka wa euro milioni 20 kusaidia kushughulikia wimbi hili jipya la wakimbizi wa Sudan kwenye mpaka wa kusini. Ninafahamu kiwango hicho hakitoshi, lakini acha na sisi angalau tuchangie sehemu ndogo ya hisani yenu" amesema Borell.

Akitoa shukrani za nchi yake kwa Umoja wa Ulaya, waziri wa mambo ya kigeni wa Misri Sameh Shoukry alisema mchango huo ni muhimu sana katika kuisaidia serikali mjini Cairo kushughulikia mzozo wa wakimbizi unaoongezeka.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW