Pande zinazopigana Yemen zabadilishana orodha ya wafungwa
19 Desemba 2018Wakati huo huo muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulishambulia kituo cha jeshi la anga katika mji mkuu unaoshikiliwa na waasi leo wakati usitishaji mapigano ukiendelea katika mji wa bandari wa Hodeida. Sekione Kitojo na taarifa zaidi.
Kundi la Wahouthi wenye mafungamano na Iran na serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia wanatarajiwa kuwaachia huru wafungwa kwa wakati mmoja mwezi ujao kama sehemu ya kujenga hali ya kuaminiana iliyofikiwa katika makubaliano katika mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa nchini Sweden.
Mkurugenzi wa kanda wa shirika la msalaba mwekundu, Fabrizio carboni, kwamba pande zinazohusika zimebadilishana orodha ya wafungwa.
"Wana wiki sita kuanzia sasa kuhakikisha kwamba orodha hizo ni sahihi na watu hao wanashikiliwa. Kwa hiyo itatuchukua hadi katika wiki ya kwanza ya januari ambako watakuwa na siku kumi kuwaachia wafungwa na kuwapeleka katika maeneo yao ya asili."
Muungano wa kijeshi
Operesheni hiyo inaulazimu muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuhakikisha kwamba anga ni salama kwa safari za ndege, amesema Carboni.
Wakati huo huo pande hizo zinazopigana zimelaumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano mjini Hodeida yaliyofikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa yenye lengo la kuepuka vita kamili kuwania udhibiti wa bandari hiyo inayotumika kwa kuingiza misaada muhimu na kusafisha njia kwa ajili ya majadiliano zaidi ya amani.
Wakaazi wameripoti kuhusu mashambulio ya anga jana Jumanne, lakini duru katika muungano unaoongozwa na Saudi Arabia zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba iwapo waangalizi wa kimataifa hawatawekwa mjini Hodeida hivi karibuni, makubaliano hayo ya kujenga kuaminiana huenda yakashindwa.
Hodeida, bandari kuu inayotumika kuwalisha watu milioni 30 wa Yemen, imekuwa lengo la mapigano mwaka huu, na kuzusha hofu nje ya nchi hiyo kwamba iwapo vita kamili vikitokea inaweza kuzuwia watu milioni 15.9 kupata mahitaji yao na kusababisha matatizo makubwa na njaa.
Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre/afpe
Mhariri: Mohamed Khelef