Amnesty International: Jeshi na M23 wakiuka sheria ya vita
20 Januari 2025Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na waasi wa M23, huenda wamekiuka sheria za vita kwa kuyashambulia maeneo yenye msongamano wa raia.
Taarifa ya Amnesty International iliyotolewa Jumatatu imeeleza, zaidi ya raia 100 waliuwawa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024.
Kulingana na ripoti hiyo, Jeshi la Kongo pamoja na waasi wa M23 wanahusika na ongezeko la matumizi ya silaha zisizo sahihi.
Tangu kundi la M23linalodai kuwalinda watu wa jamii ya Watutsi lilipoibuka tena mwishoni mwa mwaka 2021 likisaidiwa na wapiganaji wa Rwanda, limefanikiwa kuyateka maeneo mengi ya Mashariki kwa Kongo yenye utajiri wa madini na kusababisha mgogoro wa kiutu na maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeongeza kuwa mashambulizi hayo yaliyowauwa zaidi ya raia 100 na kuwajeruhi mamia wengineyalikiuka sheria ya kimataifa ya kiutu na kuna uwezekano kuwa yalikuwa uhalifu wa kivita.