1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa aiombea amani Sri Lanka

14 Januari 2015

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani alitembelea eneo la Kaskazini na kuwatolea mwito wasri-Lanka kusameheana baada ya zaidi ya miongo miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Papa Francis akiongoza misa mjini Colombo Jumatano 14.01.2015
Papa Francis akiongoza misa mjini Colombo Jumatano 14.01.2015Picha: Reuters/D. Liyanawatte

Papa Francis ameongoza ibada maalum katika eneo la Madhu lililoko kilomita 320 kaskazini mwa mji mkuu. Eneo hilo lilikuwa kitovu cha mapigano makali kati ya wapiganaji wakitamil na jeshi la Sri Lanka kwa miaka 26.Watu zaidi ya 100,000 waliuwawa kabla ya vita kumalizika mwaka 2009.

Ibada iliyoongozwa na papa Fransis imefanyika katika kanisa katoliki lenye umri wa miaka 400 wakihudhuria zaidi watu wa jamii ya wachache ya watamil.Ingawa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 26 kati ya jamii ya waliowengi ya Sinhalese na wapiganaji wanaopigania kujitenga wa kitamil vilimalizika mwaka 2009 bado hali ya mvutano na wasiwasi nchini humo bado ipo kati ya jamii ya waliowengi ya Sinhalese na makundi ya jamii za wachache. Kutokana na hali hiyo papa Francis ameiombea amani nchi hiyo akisema katika juhudi ngumu za kutafuta amani na kusameheana mama maria yaani mama wa yesu Kristo daima yuko kwa ajili ya kuwapa moyo watu kuwaongoza na kuwatangulia.

Mapema hii leo kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani alimtangazakasisi mmishionari wa karne ya 17 Joseph Vaz kuwa mtakatifu wa kwanza nchini Sri Lanka katika misa maalum iliyohudhuriwa na zaidi ya watu laki 5 kwenye viwanja vya ufukwe wa bahari vya Galle Face mjini Colombo.Papa alisema Joseph Vaz alifahamu jinsi ya kutangaza ukweli na uzuri wa neno la injili katika muktadha wa dini nyingi kwa heshima,kujitolea,kuvumilia na busara.

Waumini wa kikatoliki waliojitokeza katika misa ya papa FrancisPicha: Reuters/S. Rellandini

Halikadhalika ametolea mwito wakristo nchini Sri Lanka kuiga mfano wa maisha ya mtakatifu huyo mpya na kutumia mfano huo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta amani,haki na maridhiano katika jamii.

Mamia kwa maelfu ya waumini walisubiri usiku kucha katika viwanja vya fukwe ya bahari kupata nafasi ya kuhudhuria misa hiyo maalum iliyofanyika leo.Katika kutambua umuhimu wa ziara hiyo ya papa Francis Serikali ya Sri Lanka leo imewaachia huru wafungwa kiasi ya 600 na wengine kupunguziwa adhabu ya kifungo kama ishara ya kuadhimisha ziara hiyo.

Ikumbukwe kwamba Papa Francis aliwasili Sri Lanka jana Jumanne na kumtembelea rais mpya Maithripala Sirisena kabla ya kukutana na viongozi wa kidini wa kibudha,Hindu,waislamu na wakristro mjini Colombo.Papa Francis ataelekea Ufilipino hapo kesho alhamisi ambako anatarajiwa kubakia hadi siku ya Jumatatu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW