Papa aitaka Ulaya kufanya zaidi kutatua matatizo ya dunia
2 Agosti 2023"Unaelekea wapi ikiwa haupendekezi kwa ulimwengu njia ya amani, njia bunifu za kukomesha vita nchini Ukraine na migogoro mingi inayochafua dunia kwa damu?" Papa Francis alisema katika hotuba yake wakati wa chakula cha mchana kwa wawakilishi wa serikali ya Ureno na mashirika ya kiraia katika Kituo cha Utamaduni cha Belém mjini Lisbon.
Katika hotuba yake kuu ya kwanza kwa umma wakati wa ziara yake ya sasa nchini Ureno, mzee huyo mwenye umri wa miaka 86 alishutumu kutokuwepo kwa mpango wa amani wa kijasiri na kusema pesa nyingi zinawekezwa katika silaha kuliko siku zijazo za watoto.
Ulaya pia ilipaswa kukabiliana na matatizo yake, Papa alionya. Alikosoa ushughulikiaji wa wahamiaji katika mipaka ya nje ya bara hilo na katika Bahari ya Mediterania, kupungua kwa viwango vya kuzaliwa pamoja na majadiliano juu ya euthanasia.
"Udhalimu wa kimataifa, vita, hali ya hewa na migogoro ya uhamiaji vinakua kwa kasi zaidi kuliko uwezo na mara nyingi nia ya kukabiliana na changamoto hizi pamoja", Francis alisema.
Soma pia:Papa Benedicto wa XVI na njia ya amani kuisuluhisha mizozo
Badala yake, papa ana ndoto ya "Ulaya inayoongoza mataifa ya Magharibi" ambayo inatumia ustadi wake kutuliza maeneo yenye vita na kuwasha mwanga wa matumaini. Bara hilo linaweza kuwa dereva wa "ufunguzi wa kimataifa" unaohitajika ulimwenguni. Ulimwengu unaihitaji Ulaya - "Ulaya halisi" - kama mjenzi wa daraja na mtunza amani.
Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki yuko Ureno kwa siku tano kuadhimisha Siku ya Vijana wa Kanisa Katoliki Duniani (WYD) 2023. Baada ya kuwasili Lisbon, Francis alikaribishwa na Rais wa Ureno Marcelo Rebelo de Sousa katika makazi yake, Belém Palace, kwa sherehe rasmi ya makaribisho.
Katika ujumbe wake katika Kitabu cha Heshima cha Ureno, Francis alisema: "Kama mhujaji wa matumaini nchini Ureno, ninaomba na kutumaini kwamba nchi hii yenye moyo wake mchanga itaendelea kufikia upeo wa udugu."
Alisema anatumai Lisbon itaonyesha njia za kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na "maswali na matatizo makubwa ya Ulaya na dunia."
Katika Ubalozi wa Vatikani mjini Lisbon, makao rasmi ya kitume, papa anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu António Costa na baadaye anatarajiwa kusali sala ya jioni katika Monasteri ya Jerónimos ya mji huo, iliyopewa jina hilo kutokana na ukweli kwamba ilikuwa inakaliwa na watawa kutoka dhehebu la Mtakatifu Jerome.
Mambo makuu ya safari yake ni pamoja na mikutano na vijana wagonjwa kwenye patakatifu pa Fátima, ambapo anatarajiwa pia kusali kwa ajili ya amani, pamoja na sala ya jioni Jumamosi na Misa Jumapili.
Chanzo: DPAE