Papa ajisikia "aibu" vijana kurithi dunia iliyogawika
31 Machi 2018Akizungumza mjini Roma mwishoni mwa utamaduni wa vituo vya Ijumaa kuu katika njia inayopita msalaba, kiongozi huyo wa kidini alisema dunia "inatafunwa na ubinafsi ambamo vijana, wagonjwa na wazee wanatengwa".
Huku kukiwa na ulinzi mkali, kiasi ya waumini 20,000 , wengi wao wakibeba mishumaa, walikusanyika kuzunguka ukumbi wa kale wa makumbusho mjini Roma kwa ajili ya kanuni hiyo ya kidini ambayo ni kurudiwa kwa njia ambayo Yesu alipitia kuelekea katika kusulubiwa. Mji mkuu wa Italia umewekwa katika uangalizi mkubwa kufuatia wiki ambayo iligubikwa na wimbi la kukamatwa kwa watu wanaosadikiwa kuwa ni magaidi.
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Marco Minniti alionya wiki hii kuhusu kitisho cha hali ya juu cha shambulio nchini italia, na kiasi ya polisi 10,000 waliwekwa kuhakikisha usalama mjini Roma, hususan wakati wa sikukuu ya pasaka zinazosimamiwa na papa mwishoni mwa juma hili na kufikia kilele kwa sherehe za Pasaka siku ya Jumapili.
Papa aliwaongoza Wakatoliki katika sala ya Ijumaa kukiwa na ulinzi mkali , na kuwataka watu, ikiwa ni pamoja na viongozi katika kanisa, kutafakari kiwango cha kujisikia aibu kwa jukumu walilonalo katika madhila ya dunia.
Tujisikie aibu
Francis alielekeza matamshi yake, aliyotoa mwishoni mwa njia hiyo ya msalaba huku watu wakiwa wameshika mishumaa, katika muktadha wa kujisikia aibu na kutubu, kulikonasibishwa na taswira ya dunia ya kisasa ambako, fahari, kiburi na ubinafsi mara nyingi hukandamiza ubinadamu na ukarimu.
Akizungumza kwa sauti ya unyenyekevu, alizungumzia kuhusu "aibu kwa sababu watu wengi, hata baadhi yenu , watumishi wa Mungu , wamejiweka kuamuliwa na matamanio na sifa ya ushindi, na hivyo kupoteza thamani yake."
Tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, Francis mara nyingi amewataka mapadre na maaskofu wa Katoliki kuishi maisha ya kawaida, kuwatumikia wengine, na sio kutafuta ukubwa katika kanisa ama katika jamii kwa jumla.
Ijumaa Kuu siku ya utulivu na unyenyekevu mkubwa katika kalenda ya Wakristo, ni kumbukumbu ya siku Biblia inasema Yesu alisulubiwa. Njia ya msalaba ina matukio 14, yanayoitwa vituo, kutoka enzi za gavana wa Roma Pontius Pilate alipomhukumu Yesu kifo hadi kuzikwa kwake katika kaburi.
Francis amesema watu wengi duniani hii leo wanapaswa kujisikia "aibu kwa kupoteza hisia za aibu", na kuongeza kwamba aibu inaweza kuonekana kuwa " hisani 2 kutoka kwa Mungu. Amesema wengi wanapaswa kujisikia aibu kwa sababu kizazi chetu kinawaacha vijana katika dunia ambayo imepata nyufa kwa migawanyiko na vita, dunia iliyotafunwa na ubinafsi..
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre, afpe
Mhariri: Daniel Gakuba