1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa akubali kadinali Theodore McCarrick ajiuzulu

28 Julai 2018

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amekubali uamuzi wa kujiuzulu wa kadinali wa Marakeni Theodore McCarrick kwenye baraza la makadinali kutokana na madai ya kumdhalilisha kingono mvulana wa miaka 11.

USA | Kardinal Theodore Edgar McCarrick sexuellen Missbrauchs beschuldigt
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Franklin

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki dunani alichukua hatua haraka mara tu baada ya kupokea barua ya kujizulu ya kadinali Theodore McCarrick hapo jana. Mnamo mwezi wa Juni Theodore McCarrick aliyekuwa askofu wa Washington alivuliwa mamlaka ya ukasisi baada ya baraza la uchunguzi kubainisha kwamba palikuwapo ushahidi thabiti wa kuonyesha kwamba alimdhulumu mvulana huyo mwenye umri wa miaka 11. McCarrik mweye umri wa miaka 88 ni miongoni mwa makadinali maarufu duniani na kiongozi wa dini wa ngazi ya juu kuwahi kukabiliwa mashtaka ya udhalilishaji wa kingono .

Hata hivyo mashtaka hayo yanayotokana na tukio la miaka 40 iliyopita. Anadaiwa alimshikashika mvulana aliyekuwa na umri wa miaka 11 wakati huo katika jiji la New York. Mtu huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 51 amesema uhusiano wakudhalilishwa kingono uliendelea kati yake na Askofu huyo kwa muda wa miaka miwili. Lakini McCarrik amekanusha madai ya awali.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki amechukua hatua haraka kutekeleza ahadi aliyotoa ya kutovumilia tabia ya kufichiana siri miongoni mwa makasisi. Madai ya udhalilishaji wa kingono yanawakabili makasisi wengi ikiwa pamoja na maaskofu na makadinali ikiwa pamoja na kadinali wa Australia George Pell ambaye ni mmoja wapo wa washauri  wa ndani wa baba mtakatifu. Yeye pia anakabiliwa na mashtaka ya udhalilishaji wa kiongono nchini mwake.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa FrancisPicha: Getty Images/AFP/F. Tiziana

Uamuzi wa baba mtakatifu unathibitisha kwamba sasa anachukua hatua baada ya madai kutolewa. Kuhusu mkasa wa kadinali wa Scotland Keith O Brien aliedaiwa kuwanyanyasa kiongono  watawa, baba mtakatifu aliridhika baada ya kadinali huyo kujiuzulu, licha ya uchunguzi kufanywa na mwendesha mashtaka mwandamizi wa Vatican. Lakini sasa baba Mtakatifu Francis anamchukulia hatua thabiti kadinali McCarrick, ingawa madai yanayomkabili bado hayajachunguzwa.

Kasisi wa chuo kikuu cha Kanisa Katoliki Kurt Martens ametilia maanani kwamba hii ni mara ya kwanza kwa baba mtakatifu kumwamrisha mtuhumiwa kufunga sala ya kutubu. Maaskofu kadhaa wamekabiliwa na tuhuma za udhalilishaji wa kingono kwa muda wa miaka mingi, madai yaliyolitia dosari kanisa Katoliki. Lakini kanisa hilo lilitumia mbinu ya kuwahamisha tu watu hao.

Mapema mnamo mwezi huu Askofu wa Australia alishtakiwa na kuhukumiwa baada ya kuthibika kwamba alificha uchafu wa udhalilishaji wa kingono. Kasisi huyo mwandamizi alipewa adhabu ya kuwekwa mahabusi kwa muda wa miezi 12.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Yusra Buwayhid