1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa atoa wito wa dunia bila silaha za kinyuklia

Sekione Kitojo
24 Novemba 2019

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis ameitaka dunia kuachana kabisa na silaha za atomiki katika hotuba yake mji Nagasaki Japan, mji  ulioshambuliwa kwa mabomu ya nyuklia mwishoni mwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Papst Franziskus in Japan
Picha: Picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

"Eneo  hili linatufanya  kutambua  maumivu na maovu ambayo sisi binadamu  tunaweza kufanyiana," Francis  alisema katika  eneo  la uwanja  wa  kumbukumbu  ya  mabomu ya  atomiki mjini Nagasaki huku  mvua  ikinyesha.

Papa Francis akiweka shada la maua katika eneo la kumbukumbu ya shambulio la bomu Nagasaki nchini JapanPicha: Picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Kabla  ya  hotuba  yake, papa alitoa heshima  zake  kwa  wahanga wa  shambulio la Marekani la  bomu la nyuklia mwaka 1945  katika mji  huo  wa  kusini  magharibi  nchini  Japan, na  kuwauwa  watu 74,000, ikiwa  ni  pamoja  na  maelfu  ya  wakatoliki.

"Hapa  katika  mji  huu ambao  ulishuhudia madhila ya  maafa  ya kibinadamu  na  mazingira kutokana  na  shambulio  la  nyuklia, juhudi zetu kuzungumzia dhidi  ya mashindano ya  silaha hazitatosha," amesema  Francis, ambaye  ameanza  ziara  yake  ya  siku  nne nchini  Japan siku  ya  Jumamosi.

Shambulio la  mji  wa  Nagasaki  Agosti 9, 1945, lilikuja  siku  tatu baada  ya  shambulio  la  kwanza  la  bomu  la  atomiki lililodondoshwa na  ndege  ya  mashambulizi  ya  B-29  ya  Marekani na  kuripuliwa katika  mji wa  Hiroshima, na  kusababisha  watu 140,000 kuuwawa.

Amani na  uthabiti

"Moja  kati  ya kile moyo  wa  binadamu inachopenda zaidi ni usalama, amani  na  uthabiti. Kuwa  na  silaha  za  nyuklia  na  silaha nyingine  za  maangamizi  sio  jibu la  hisia  hizi  moyo wa  binadamu unavyopenda, kwa kweli  kila  mara binadamu  anajaribu  kuzuwia hilo," amesema  papa  mwenye  umri  wa  miaka 82.

Pope akizungumza katika mkutano na maaskofu kutoka katika ubalozi wa Vatican mjini Tokyo, Japan, Novemba 23, 2019.Picha: Reuters/Vatican Media

"Amani na  uthabiti  wa  kimataifa hayalingana  na  majaribio  ya kujenga juu  ya hofu ya uharibifu  wa  pamoja  ama  kitisho cha maangamizi ya  jumla," amesema.

Kiongozi  huyo wa  kanisa  Katoliki  alikuwa  miongoni mwa  watu  wa kwanza  kutia  saini  na  kuidhinisha  mkataba  wa  kuzuwia  silaha za  kinyuklia, ambao  uliidhinishwa  na  mataifa  122  mwezi  Julai 2017.

Hata  hivyo, mkataba  huo  bado  haujaanza   kutumika  kwa  kuwa haujaidhinishwa  na  mataifa 50 ambayo  yanatakiwa  kutia  saini.

Wanaharakati  wa  kupinga  silaha  za  kinyuklia  wameitaka  Japan, nchi  pekee  ambayo  imeathirika  na  mashambulizi  ya  silaha  za atomiki, kutia  saini na  kuidhinisha  mkataba  huo  haraka iwezekanavyo.

Lakini serikali  ya  waziri  mkuu  Shinzo Abe hadi sasa  imekataa kufanya  hivyo  wakati  nchi  hiyo  ikiwa  chini  ya  mwamvuli  wa kinyuklia  wa  Marekani.

Papa Francis akutana na waumini wa kanisa Katoliki katika uwanja wa kumbukumbu ya shambulio la bomu la nyuklia mjini Nagasaki.Picha: Picture-alliance/AP Photo/G. Borgia

Dunia bila silaha za kinyuklia

"Nikiwa naamini kuwa  dunia  bila  silaha  za  kinyuklia inawezekana na  ni  muhimu, nawataka  viongozi  wa  kisiasa  kutosahau  kuwa silaha  hizi haziwezi kutulinda kutokana  na  kitisho cha  hivi  sasa katika  usalama  wa  kitaifa  na  kimataifa," amesema  Papa.

"Tunahitaji  kutafakari athari  za  maafa  ya  uwepo wake,hususan kutokana  na  mtazamo  wa  kiutu  na  mazingira, na  kukataa kuongeza  hofu  ya  kimazingira, kutokuaminiana na  uhasama unaochochewa  na  nadharia  za  nyuklia".

Papa  atafanya  ibada ya  misa  katika  uwanja  wa  michezo  mjini Nagasaki baadaye mchana  na  kisha  atasafiri  kwenda  Hiroshima, ambako "mkutano  kwa  ajili  ya  amani" umepangwa  kufanyika.

Papa Francis akitoa ujumbe wake katika hotuba katika uwanja wa kumbukumbu ya shambulio la bomu la atomic mjini NagasakiPicha: Reuters/I. Kato

Siku  ya  Jumatatu , Francis anatarajiwa  kufanya  mkutano  na mfalme  Naruhito, ambaye  ameingia  madarakani  Mei  mosi, na waziri  mkuu  mjini  Tokyo.

Papa  pia  atakutana  na  wahanga  wa  tetemeko  la  ardhi  la mwaka  2011, tsunami na  maafa  ya  nyuklia  kaskazini  mashariki mwa  Japan.

Ziara  yake  inakuwa  ya  kwanza  kufanywa  na  papa  nchini  Japan katika  muda  wa  miaka  38. Mwaka  1981 papa  John Paul 11 alikwenda Hiroshima, Nagasaki na  Tokyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW