1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa awatangaza John wa 23 na John wa Pili watakatifu

27 Aprili 2014

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis Jumapili(27.04.2014) amewatangaza watangulizi wake wawili John wa 23 na John wa Pili kuwa watakatifu mbele ya umati uliofurika uwanja wa kanisa la Mtakatifu Petro,Vatican.

Papa Francis akiongoza misa ya kuwatangaza John wa 23 na John wa Pili kuwa watakatifu katika kanisa la Mtakatifu Petro ,Vatican. (27.04.2014)
Papa Francis akiongoza misa ya kuwatangaza John wa 23 na John wa Pili kuwa watakatifu katika kanisa la Mtakatifu Petro ,Vatican. (27.04.2014)Picha: Reuters

Katu haikuwahi kutokea kabla kwa papa aliyoko madarakani na yule aliyestaafu kushiriki misa kwa pamoja hadharani tena katika tukio la kuwatukuza watangulizi wao wawili mashuhuri kabisa. Kuwepo kwa Benedict ni onyesho la kuweka uwiano ambalo Francis aliliwazia wakati alipoamuwa kuwatangaza kwa pamoja kuwa watakatifu John na John Paul ili kuonyesha umoja wa Kanisa Katoliki kuwatukuza mapapa hao wawili ambao walikuwa wakipendwa na wahafidhina halikadhalika wataka mageuzi.

Francis alishusha pumzi nzito na kusita kwa muda mdogo kabla ya kutowa tamko la kutangaza utakatifu kwa lugha ya Kilatin akionekana kama vile ameguswa na tukio hilo la kihistoria ambalo alikuwa analifanya.

Amesema baada ya tafakuri, mashauriano na kuomba msaada wa Mungu "tunawatangaza na kuwaelezea Wabarikiwa John wa 23 na John wa Pili kuwa watakatifu na tutawaorodhesha kuwa miongoni mwa watakatifu, kuamrisha kwamba watukuzwe kuwa hivyo na kanisa zima." Shangilio liliibuka kutoka umati ulliofurika kuanzia uwanja wa Mtakatifu Petro hadi Mto Tiber na kupindukia hapo.

Uwepo wa Benedikt

Benedict alikuwa ameketi kwenye madhabahu na makadinali wengine na aliwasili mwenyewe kwenye uwanja huo huku akishangiliwa na umma uliokuwepo akiwa amevalia mavazi meupe na kofia maalum ya maaskofu. Alisimama kumsalimia rais wa Italia na baadae Papa Francis wakati alipowasili na aliungana na wenzake kwenye kuimba nyimbo za pamoja za kidini zilizofuatia ada za kutangaza utakatifu.

Papa mstaafu Benedict wa 16 akiwasili katika kanisa la Mtakatifu Petro Vatican.(27.04.2014).Picha: FILIPPO MONTEFORTE/AFP/Getty Images

Wizara ya mambo ya ndani ya Italia ilitabiri kwamba watu milioni moja watakuwa wanaiangalia misa hiyo kutoka uwanja wa Mtakatifu Petro,mitaa inayozunguka uwanja huo na gulio zilioko karibu ambapo vionyeshoo vikubwa vya TV vimewekwa kuwezesha umati uliokuwa na shauku kulifuatilia tukio hilo.

Mahujaji wa Poland wenye bendera nyekundu za nchi hiyo alikozaliwa Papa John wa Pili walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufurika kwenye uwanja huo kabla ya hata kuchomoza kwa jua. Mmojawapo wa raia wa Poland David Halfar aliyekuwepo uwanjani hapo amekaririwa akisema "Mapapa wanne katika hafla moja ni tukio la shani kulishuhudia na kuwepo, kwa sababu ni historia inayoandikwa mbele ya macho yetu."

Wengi wa wale waliowasili mwanzo katika uwanja wa Mtakatifu Petro walikuwa wamepiga kambi usiku kucha karibu na uwanja huo wakitumia magodoro ya kutia pumzi na matandiko ya kulalia. Wengine walikuwa hawakulala kabisa na walishiriki katika ibada za mkesha kwenye makanisa kadha mjini Rome. Benedict aliahidi kuishj maisha ya faragha baada ya kujiuzulu mwaka jana,lakini Francis alimshawishi awe anashiriki hadharani shughuli za kanisa.

Umma uliofurika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Petro Vatican. 27.04.2014.Picha: Reuters

Benedict alihudhuria hafla ya mwezi wa Februari ambapo Francis aliwatawaza makadinali wapya 19.Lakini kuhudhuria misa kwa pamoja na Francis ni jambo jengine tafauti kabisa,kwanza kwa taasisi hiyo ya kanisa iliyoko kwa miaka 2,000 na ni tafakuri ya shauku ya Francis kuonyesha kuendelea kusonga mbele kwa uongozi huo wa upapa licha ya kuwepo kwa mvuto tafauti, vitu vya kupewa kipau mbele na siasa tafauti.

Watakatifu wapya

Papa John wa 23 ambaye aliongoza kuanzia mwaka 1958 hadi 1963 ni shujaa kwa Waliberali wa Kikatoliki kutokana na kule kuitisha mkutano wa Baraza la Pili la Kanisa.Mikutano hiyo imeliingiza kanisa kwenye enzi ya sasa kwa kuruhusu misa ziendeswe kwa lugha za kienyeji badala ya Kilatin na kushajiisha kuwepo kwa mazungumzo makubwa zaidi na watu wa dini nyengine hususan Wayahudi.

Picha za Papa John wa Pili (Kushoto) na Papa John wa 23.(Kulia).Picha: Reuters

Wakati wa uongozi wake wa robo karne kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 2005,John Paul wa Pili alisaidia kuanguka kwa utawala wa kikomnisti kutokana na kuunga mkono kwake vuguvugu la Solidarity nchini Poland.Uongozi wake wa kuzuru sehemu mbali mbali duniani na kuzinduwa Siku ya Vijana Duniani ambayo ni mashuhuri imetowa nguvu kwa kizazi kipya cha vijana wa Kikatoliki wakati utetezi wake wa mafundisho ya msingi ya kanisa kumewapa moyo wahafidhina baada ya vurugu za miaka ya 1960.

Therese Andjoua mwenye umri wa miaka 49 muuguzi ambaye amesafiri kutoka Libreville Gabon na mahujaji wenzake 300 akiwa amevalia vazi la Kiafrika lenye taswira za watakatifu hao wawili wapya amesema " John Paul alikuwa matumaini yetu."Amesema hapo mwaka 1962 alikwenda Gabon na wakati alipowasili aliibusu ardhi na kuwaambia inukeni,msonge mbele na msiwe na hofu kwa hiyo wakati waliposikia kwa anatangazwa kuwa mtakatifu wameinuka.

Wafalme,malkia, marais na mawaziri wakuu kutoka zaidi ya nchi 90 duniani walihudhuria hafla ya leo.Takriban viongozi 20 wa Kiyahudi kutoka Marekani, Israel,Ufaransa,Italia na nchi alikozaliwa Papa Francis yaani Argentina na Poland pia walihudhuria hafla hiyo ikiwa ni ishara ya wazi ya kuthamini hatua kubwa zilizopigwa katika uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Wayahudi chini ya John, John wa Pili na waliowafuatia kutangazwa kuwa watakatifu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri: Bruce Amani