Papa Benedicto wa XVI na njia ya amani kuisuluhisha mizozo
18 Julai 2008Katika dunia ambayo imehatarishwa na majanga na aina nyingi tu ya machafuko, viongozi wa kidini kwa kauli moja wanatoa mwito kwa viongozi wa nchi na jamii kuisuluhisha mizozo kwa njia za amani na kwa lengo la kuheshimu binaadamu, amesema Papa Benedicto wa XVI. Baba Mtakatifu ametoa mfano wa hapo hapo nchini Australia, mwenyeji wa Siku Kuu ya Vijana Duniani mwaka huu ambako amesema serikali hatimae ilikiri unyonge uliyotendewa raia asilia hapo zamani na kuanza kuchukuwa hatua kwa lengo la kufikia maridhiano chini ya msingi wa kuheshimiana na kwa maoni yake, huo ungefaa kuwa mfano:
´´Kwa sasa mnaelekea kuziba pengo lililokuwapo kati ya raia asilia na raia wengine wa Australia kwa kutilia maanani tu matarajio, elimu na maendeleo. Mfano huu unawapa matumaini raia wengine kote duniani ambao wanasubiri kuona haki zao zimeheshimiwa na jukumu lao katika jamii limetambuliwa na kuendelezwa´´.
Papa Benedicto wa XVI ameyatamka hayo baada ya kukutana kwa mazungumzo na wawakilishi wa dini za kiislamu na kiyahudi huko Australia. Amesema kwamba katika maswala yote hayo yanaohusiana na maisha ya binaadamu, dini ni kiungo na wala sio kiini cha mgawanyiko. Dini inaweza kupelekea watu wenye asili tofauti kuishi pamoja kwa amani na kujenga urafiki na majirani.
Baba Mtakatifu ameendelea kusema kuwa kanisa la kikatoliki lipo tayari kupokea maoni kutoka makanisa mengine juu ya maswala yanayotatanisha. Ni hivyo, Papa Benedicto wa XVI ameelezea wasi wasi wake juu ya mgogoro unaolikabili kanisa la kianglikana juu ya swala la kutatanisha la kuwaruhusu wanawake na mashoga kuwa padri vile vile.
Swala jingine linalomshughulisha pia kiongozi wa kanisa la kikatoliki na ambalo huenda akaliombea tena radhi katika hotuba yake nyingine iliyopangwa hapo kesho, ni tabia mbaya ya ukatili wa ngono kwa kuwashirikisha watoto ambapo baadhi ya mapadri walihusika akiwemo moja mjini Sydney Australia ambako kunafanyika shughuli kuhusiana na Siku Kuu hiyo ya Vijana duniani.
Mbali na tukio hilo la ngono, Australia inaelekea kumpata Mtakatifu wake wa kwanza, MacKillop ambae anajulikana sana kwa shughuli zake za kibinaadamu kwa ajili ya watoto katika maeneo ya vijijini nchini Australia katika karene iliyopita na jina lake kupewa kanisa moja hapo mjini Sydney. Baba Mtakatifu amesema akilitembelea kanisa hilo kuwa kunafanyika uchunguzi wa mwisho kumtangaza MacKillop mtakatifu.