1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa - Bush Walivyotofautiana juu ya Hukumu ya Kifo

Lillian Urio15 Aprili 2005

Rais George W. Bush wa marekani ndiye rais wa kwanza wa nchi hiyo kuhudhuria mazishi ya Papa na alimsifu Papa Yohana Paulo II kuwa mtetezi wa maisha ya watu, lakini viongozi hawa wawili walitofautiana katika suala la hukumu ya kifo.

Rais Bush akimsalimia Hayati Papa, Vatican, Juni 4, 2004
Rais Bush akimsalimia Hayati Papa, Vatican, Juni 4, 2004Picha: AP

Papa Yohana Paulo II alipinga hukumu ya kifo na alitumiwa wadhifa wake dhidi ya hukumu hiyo, wakati huo huo Rais Bush alikuwa ana unga mkono hukumu ya kifo na akatumia suala hili kusaidia kampeni zake za kuwania uraisi.

Wataalam wa mambo wamesema viongozi hawa walitofautiana juu ya suala hili wakati Rais Bush akiwa Gavana wa jimbo la Texas na pia alivyokuwa Rais. Lakini kifo cha Papa kilimwezesha Rais Bush kuonyesha kwamba alikubali uongozi wa Yohana Paulo wa miaka 26 na hivyo kuheshimika kisiasa.

Rais Bush alivyokuwa gavana wa jimbo la Texas, kati ya 1995 na 2000, watu 152 waliuwawa baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo. Idadi hii ya utoaji wa hukumu ya kifo ndio iliyoongoza ukilinganisha na idadi za magavana wengine katika historia ya karibuni ya Marekani.

Wakati huo huo Papa alikuwa akipinga hukumu ya kifo na alijaribu kulihusisha kanisa ili limuunge mkono.

Hotuba ya mwaka wa 1999, alioisoma mjini St. Louis Marekani, Papa alisema hukumu ya kifo ni ukatili na hatuitaji, na akasema sasa hivi inatambulika kuwa, hairuhusiwi kumnyima mtu uhai wake, hata kama mtu huyo ametenda maovu makubwa.

Angalau mara mbili Papa alimwomba Gavana Bush asimamishe mauaji huko Texas. Mwaka wa 1998 alimwomba amsamehe muuaji aliyeokoka Karla Faye Tucker.

Gavana Bush alikataa kwa sababu ingawa anajivunia ukristo wake, pia anafahamu kura zinaonyesha kwamba theluthi mbili ya Wamarekani wanaunga mkono hukumu ya kifo. Februari 3, 1998, Tucker alidungwa sindano ya sumu. Alikuwa mwanamke wa kwanza kuuwawa katika jimbo hilo tangu mwaka 1863.

Miaka mitatu baadaye, katika mkutano wao wa kwanza baada Bush kuwa Rais, Papa akamlaumu akimwambia, nchi iliyo huru na yenye maadili mema, kama ambavyo Marekani ina lenga kuwa hivyo, ni lazima ikatae matendo ambayo haya thamani na yana kiuka haki za binadamu tangu mtu anapo zaliwa hadi kufa kwake.

Rais Bush Alhamisi hii alisema ana msimamo na fikira zake. Anaamini kwamba hukumu ya kifo, ikitumika ipasavyo, inaokoa maisha ya wengine. Ndio maana anaona hamna upingamizi na imani yake, Rais Bush alisema hayo wakati akijibu swali katika mkutano na wahariri wa magazeti ya Kimarekani.

Baada ya mazishi ya Papa, Rais Bush alimzungumzia Yohana Paulo kwa heshima na akasisitiza jinsi walivyo ungana mkono katika maswala ya utamaduni wa maisha, lakini hakutaja hukumu ya kifo.

William Martin, profesa wa sosiolojia katika chuo cha Rice na mwandishi wa kitabu kinachoitwa, "Mungu akiwa upande wetu: Kukuwa kwa dini ya itikadi kali Marekani" amesema inawezekana Rais Bush alivutiwa kweli na Yohana Paulo, lakini ni wazi kwamba yale mazuri aliyoyasema juu ya Papa yamemletea sifa kisiasa.

Profesa Martin amesema Rais Bush ameweza kuwavutia wamarekani milioni 67 walio wakatoliki, ambao kwa miaka mingi sasa, chama chake cha Republican kimekuwa kikijaribu kuwavutia. Pia alimsifu Papa ambaye msimamo wake wa kupinga ukomunisti na utoaji mimba ulimfanya awe na wafuasi wengi wa kikristo wenye msimamo wakihafidhina, ambao wanamuunga mkono Rais Bush.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW