1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Frances awasili Ireland akiwa na masikitiko

Yusra Buwayhid
25 Agosti 2018

Baada ya kuwasili Ireland Jumamosi, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amesema anahuzunishwa na kushindwa kwa kanisa hilo kushughulikia tatizo la unyanyasaji wa kingono wa watoto unaofanywa na mapadri.

Irland | Besuch Papst Franziskus
Picha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire/Y. Mok

Akiwa katika Kasri la Dublin, Papa Frances amesema naye pia anahisi maumivu na aibu juu ya kushindwa kwa mamlaka ya Kanisa Katoliki kushughulikia kashfa hiyo ya kunyanyaswa kingono watoto.

"Kushindwa kwa mamlaka ya kanisa - maaskofu, wakuu wa kidini, makuhani na wengine - kushughulikia uhalifu kumesababisha hasira na bado ni chanzo cha maumivu na aibu kwa jumuiya ya Kikatoliki, "amesema Frances akiwa katika Kasri la Dublin alipokutana na Waziri Mkuu Leo Varadkar. 

Francis atakutana na wahanga wa unyanyasaji wa kingoni unaofanywa na mapadri wa kanisa katoliki, wakati wa ziara yake hiyo ya masaa 36 nchini Ireland. Ni mara ya kwanza katika kipindi cha miongo minne kwa papa wa Kanisa Katoliki kuizuru Ireland. Mamlaka ya Vatican imesema ziara hiyo itatoa fursa nyingi za kuweza kulijadili tatizo la unyanyasaji wa kingono linaloendelea katika kanisa Katoliki. 

Ingawa watu 600,000 wanatarajiwa kuhudhuria Misa itakayoongozwa na Frances Jumapili, idadi hiyo ni kidogo ikilinganishwa na miaka 40 iliopita.

Zaidi ya thuluthi tatu ya idadi jumla ya watu wa Ireland ilimiminika barabarani kumuona Papa John Paul II mwaka 1979, katika wakati ambapo talaka ya ndoa pamoja na utumiaji wa njia za uzazi wa mpango vilikuwa ni vitu visivyoruhusika nchini humo.

Mabadiliko ya Ireland

Leo hii, Ireland sio tena nchi inayoongozwa kwa misimamo ya Kikatoliki, na katika miaka mitatu iliyopita wapiga kura wameidhinisha utoaji mimba pamoja na ndoa za jinsia moja kupitia kura za maoni, hatua zote zikiwa ni kinyume na mafundisho ya madhehebu ya Kikatoliki.

Idadi ya watu wataokakusanyika barabarani au kuungana na Papa Frances katika sala ya pamoja, inatarajiwa kuwa robo tu ya watu milioni 2.7 waliompokea John Paul II mwaka 1979. Hali hiyo inaashiria jinsi gani ufuasi wa Kanisa Katoliki umepungua, tokea kudhihirika kwa visa vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto katika miaka ya 1990.

"Papa anafanya kila awezalo kushughulikia mgogoro unaoendelea kulikabili kanisa Katoliki," anasema Milena Pereira. Msichana wa Kikatoliki wa miaka 20 ambae amekuja Ireland kutoka Ureno kumuona Frances. Anatumai kutakuwapo na mageuzi - kwamba Papa atateua watu wenye misimamo kama yake katika nafasi za ngazi za juu, na kuleta mabadiliko ya haraka. "Kama atakuwapo kwa miaka mengine mitano, nadhani tutakuwa na kanisa jingine kabisa," anasema Pereira.

Papa Frances akiwa na Waziri Mkuu wa Ireland Leo VaradkarPicha: Reuters/S. Rellandini

Na ingawa maelfu ya watu wamesafiri kutoka nchi tofauti kuja kumuona Francis, Ireland si tena taifa lenye ufuasi mkubwa wa Kikatoliki kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

"Kanisa Katoliki bado ni sehemu ya jamii yetu, lakini sio kitu muhimu kuliko vyote katika maisha yetu kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita," Waziri Mkuu Leo Varadkar, aliechaguliwa mwaka jana kuwa kiongozi wa kwanza shoga nchini humo, ameliambia shirika la habari la Uingereza la BBC kabla ya ziara ya Frances.

"Ireland imebadilika na kuwa nchi nyingine kabisa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, na uhusiano wetu na Kanisa Katoliki umebadilika hasa kutokana na madhihiriko mengi kuhusu unyanyasaji wa kingono wa watoto katika kanisa hilo."

Waumini walipa mgongo Kanisa Katoliki

Kuporomoka kwa ufuasi wa Kanisa Katoliki nchini Ireland kulianza katika miaka ya 1990, pale kashfa ya kwanza ya unyanyasaji wa kingono uliofanywa na padri ilipodhihirika. Mwanzo waumini wa Kikatoliki wa Ireland hawakustushwa sana: Mnamo mwaka 1992 ilijulikana kwamba Askofu wa Galway, Eamon Casey, alikuwa na mtoto wa miaka 17. Kufuatia kashfa hiyo, Casey alijiuzulu kutoka katika wadhifa huo na kwenda Amerika Kusini kwa kazi ya umishionari.

Hata hivyo, hilo lilifuatiwa na msururu wa ripoti kuhusu unyanyasaji wa kingoni katika shule za Kikatoliki, nyumba za kulelewa watoto na taasisi nyenginezo za Kikatoliki. Raia wa Ireland walishtushwa na hali hiyo. Wengi walilipa mgongo Kanisa Katoliki baada ya uchunguzi kuthibitisha kwamba viongozi wa ngazi za juu katika kanisa hilo wamekuwa wakiwalinda mapadri wanaofanya vitendo hivyo na kuwahamishia katika dayosisi nyengine, ambako waliweza kufanya vitendo vibaya zaidi. Kati ya mwaka 2005 na 2011 idadi ya watu wanaokwenda kanisani imepungua kwa asilimia 20.

Tokea wakati huo kanisa Katoliki limepoteza ushawishi wake, sio tu kama mamlaka ya kidini lakini pia kama mamlaka ya kisiasa. Licha ya upinzani mkubwa kutoka kanisa hilo, Mei 2015 Ireland ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuhalalisha ndoa za jinsia moja kupitia kura ya maoni, iliyoshinda kwa wingi mkubwa. Hii ni nchi ambayo ushoga ulifutwa kuwa sio tena kosa la jinai mwaka 1993.

Ndani ya kizazi kimoja Ireland imebadilika kutoka nchi yenye misimamo ya kihafidhina na kuwa nchi ya kiliberali.

Kukutana na viongozi wa Ireland

Papa Frances aliwasili asubuhi Jumamosi mji mkuu wa Dublin nchini Irealnd. Alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Simon Conevey, watoto wake waliomkabidhi Frances mauwa, pamoja na maaskofu kadhaa wa Ireland.

Papa ataanza ziara yake ya siku mbili kwa kukutana na rais wa Ireland Michael D. Higgins pamoja na Varadkar, ambaye amesema atajaribu kumshinikiza Francis kuhitahidi kuchukua hatua zaidi katika kuushughulikia mgogoro huo wa unyanyasaji wa kingono.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/dpa/reuters/DW

Mhariri: Gamba, Isaac

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW