1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ahimiza amani ujumbe wa Pasaka

31 Machi 2024

Papa Francis ameuhimiza ulimwengu upinge mantiki ya silaha katika ujumbe wake wa Pasaka katika makao makuu ya kanisa Katoliki Vatican.

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, katikatiPicha: Yara Nardi/REUTERS

Katika hotuba yake ya kitamaduni inayopeperushwa kote ulimwenguni, papa Francis amelaani vita akivitaja kuwa siku zote ni upuuzi na kushindwa, akigusia mizozo nchini Ukraine, Gaza, Sudan, Myanmar na kwingineko.  

Papa amerudia tena wito wa mapigano yasitishwe Gaza, akitaka misaada zaidi ipelekwe katika eneo hilo na mateka waachiwe huru waliotekwa na kundi la Hamas wakati wa shambulizi la Oktoba 7 mwaka uliopita dhidi ya Israel lililosababisah vita hivyo. 

"Tusiruhusu upepo wa vita uvume Ulaya na eneo la Mediterania. Tusikubali mantiki ya matumizi ya silaha na kujihami tena na silaha," aliongeza. 

Papa Francis amependekeza mabadilishano ya wafungwa wote kati ya Urusi na Ukraine huku vita kati ya nchi hizo mbili vikiingia katika mwaka wake wa tatu. 

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani pia amewahimiza viongozi wa dunia wafanye juhudi kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na kuwaokoa wahanga. 

Papa aongoza misa ya Pasaka

Hapo kabla, Papa Francis ameongoza misa ya Jumapili ya Pasaka katika uwanja wa Mtakatifu Petro Jumapili asubuhi huku ulinzi ukiimarishwa na mamlaka za Italia.

Huku Francis akiwepo, padri wa cheo cha juu aliongoza misa hiyo kwa niaba ya papa huyo mwenye umri wa miaka 87, ambaye hali yake ya afya ni dhaifu.

Uwanja wa Mtakatifu PetroPicha: Marco Iacobucci/ipa-agency/picture alliance

Waumini kiasi 30,000 walihudhuria misa hiyo, viwango vya joto vya msimu wa machipuko vikiwa kiasi nyuzi 20 katika kipimo cha Celcius lakini hali hii ya hewa ikiandamana na upepo mkali.

Uwanja wa Mtakatifu Petro umerembeshwa kama kawaida kwa maua na mimea, mingi kutokea Uholanzi.

Kulikuwa na kelele za shangwe wakati papa Francis alipopitishwa kando ya umati wa watu akiwa kwenye gari lake la kipapa baada ya misa, huku wengi wakipiga kelele: "Viva il Papa!" Papa aishi muda mrefu.

Soma pia: Papa Francis asema vita ni uhalifu dhidi ya ubinadamu

Maadhimisho ya Pasaka ya Vatican yamegubikwa na wasiwasi kuhusu kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani ambaye hali yake ya afya imekuwa mbaya kwa miezi kadhaa.

Usalama waimarishwa

Usalama uliimarishwa kama ilivyo ada kila mara, lakini umeimarishwa zaidi mwaka huu kufuatia shambulizi la kigaidi kwenye ukumbi wa tamasha karibu na mji wa Moscow nchini Urusi, ambalo kundi la kigadi lenye makao yake nchini Afghanistan, Islamic State Khorasan Province, Dola la kiislamu mkoa wa Khorasan (USKP) limedai kuhusika.

Kumekuwa na foleni ndefu kwenye malango ya kuingilia uwanja wa Mtakatifu Petro wakati polisi wa Italia walipofanya upekuzi.

Misa ya leo, iliyofuatiwa na ujumbe wa kitamaduni wa baraka ya "Urbi et Orbi" - maneno ya lugha ya kilatini yenye maana kwa mji na ulimwengu - ni tukio muhimu la likizo ya Pasaka na ndilo tamasha muhimu katika kalenda ya Kikristo.

Katika Jumapili ya Pasaka, wakristo husherehekea ufufuo wa Yesu Kristo na hivyo ushindi wa uzima dhidi ya kifo.

Baada ya misa, kiongozi huyo wa kanisa Katoliki aliingia kanisa la Mtakatifu Petro na kutoa ujumbe wa pasaka na baraka wa "Urbi et Orbi".

(afp,dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW