1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ahimiza jamii za Iraq kuvumiliana

Sylvia Mwehozi
5 Machi 2021

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili mjini Baghdad na kukutana na rais wa taifa hilo Barham Salih pamoja na maafisa wengine wa serikali na kutoa wito wa kukumbatia mitizamo tofauti na jumuishi. 

Vatikan Petersdom Papst Franziskus Segen "Urbi et orbi"
Picha: Vatican Media/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amewasili mjini Baghdadna kukutana na rais wa taifa hilo Barham Salih pamoja na maafisa wengine wa serikali na kutoa wito wa kukumbatia mitizamo tofauti na jumuishi. 

Papa Francis aliwasili mchana wa leo katika taifa hilo lililokumbwa na vita, ikiwa ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi wa juu wa Kanisa katoliki, na kupuuzia kitisho cha usalama na janga la virusi vya corona.

Maafisa wa usalama walipeperusha bendera za Iraq na Vatican na kisha kulisindikiza gari lililombeba Papa Francis hadi kwenye eneo lenye majengo muhimu ya serikali na balozi za nchi tofauti. Rais wa Iraq Barham Salih alimsalimu Papa Francis nje ya ikulu ambapo viongozi wote wawili walivalia barakoa wakati nyimbo za taifa za Iraq na Vatican zikipigwa. Kabla ya kuwasili Ikulu, Papa Francis aliusalimu umati wa watu waliojitokeza kumlaki wakati akipita katikati ya mji wa Baghdad.

Bango linalomwonyesha Papa Francis na kiongozi wa Kishia Ayatollah Ali SistaniPicha: SABAH ARAR/AFP via Getty Images

Francis amemueleza rais Salih na maafisa wengine kuwa hakuna mtu anayepaswa kuchukuliwa kuwa mwananchi wa ngazi ya pili. Amesema Wairaq wa imani zote wanastahili kuwa na haki sawa na ulinzi kama ilivyo kwa idadi kubwa ya Waislamu wa kishia. "Ni ikiwa tu tutajifunza kuondoa tofauti zetu na kuona kila mmoja kama mwanafamilia tutatengeneza ulimwengu bora wa kizazi kijacho".

"Kwa miongo kadhaa iliyopita, Iraq imepata athari mbaya za vita, janga la ugaidi na mizozo ya kidini mara nyingi imewekwa katika misingi inayozuwia watu kuishi pamoja kwa amani kwa makundi tofauti ya kikabila na dini, maoni na tamaduni tofauti. Yote hii imeleta uharibifu "

Kwa upande wake rais Salih amesisitiza kuwa Mashariki ya kati inakabiliwa na "mgogoro wa kuishi pamoja" kwasababu ya mivutano ya kikanda na ugaidi. Ameongeza umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani na uhifadhi wa karibu miaka 2000 ya jamii ya Kikristo ya Iraq. Rais huyo amesema "Mashariki ya Kati haiwezi kufikirika bila ya Wakristo" na kwamba kuondoka kwao kunaweza kuwa na athari kubwa.

Ziara hiyo ni ya kwanza kufanywa na Papa katika taifa hilo la Mashariki ya Kati. Mamlaka za Iraq zinatumai kuelezea hali ya usalama iliyoimarika hasa baada ya kulifurusha kundi linalojiita dola la Kiislamu IS mwaka 2017. Licha ya hofu ya usalama na janga la virusi vya corona Papa Francis ameizuri Iraq kujaribu kuhamasisha idadi ndogo ya wakristo inayozidi kupungua, ambao waliteswa na kundi la IS na kuendelea kubaguliwa na jamii kubwa ya Washia.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW