1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ahimiza masikizano na kuvumiliana Indonesia

4 Septemba 2024

Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amehimiza masikizano na kuishi kwa kuvumiliana nchini Indonesia, taifa kubwa zaidi la Waislamu duniani, ambalo limekuwa kituo cha kwanza cha ziara yake barani Asia.

Indonesia | Papa Francisi na Joko Widodo
Rais Joko Widodo wa Indonesia na Papa Francis wakijadili amani ya dunia. Septemba 04, 2024 mjini Jakarta.Picha: Muchlis Jr/Indonesia Presidency

Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameitolea mwito Indonesia kutimiza ahadi yake ya kuweka mazingira ya kuwepo masikizano baina ya watu wa imani na tamaduni tofauti na kuimaliza hali ya kukosekana uvumilivu wa kidini nchini humo.

Kiongozi huyo wa kidini ametowa mwito huo wakati akianza ziara yake ya siku 11 katika mataifa manne ya Kusini Mashariki mwa Asia na kanda ya Kusini mwa Bahari ya Pasifiki.

Soma pia:Papa Francis aanza ziara ndefu zaidi ya nje

Alikutana na rais anayeondoka madarakani Joko Widodo pamoja na rais mteule Prabowo Subianto katika kasri la rais. Katika mazungumzo yake na viongozi hao wa Indonesia, Papa Francis aliyazungumzia maingiliano ya kibinadamu katika visiwa 17,000 vya nchi hiyo na kusema kila kisiwa kina nafasi yake katika kuleta mshikamano wa taifa hilo.

Papa awaasa vijana Kongo

01:55

This browser does not support the video element.

“Masikizano katika jamii ya tamaduni mbalimbali yanafikiwa ikiwa kuna mwelekeo maalum utakaozingatia mahitaji ya pamoja na ikiwa kila jamii na kila dini itachukuwa hatua ya kuwa na moyo wa  kutafuta maslahi ya pamoja ya kuleta mafanikio kwa kila mmoja,'' alisema Papa.

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani pia ameonya kwamba uwepo wa tamaduni mbalimbali unaweza pia kuwa chanzo cha migogoro, akigusia mifano iliyoshuhudiwa hivi karibuni ya kutokuwepo uvumilivu  nchini Indonesia pamoja na wasiwasi kuhusu migogoro inayoendelea duniani.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW