1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapadri 14 wa Kikatoliki watiwa mbaroni nchini Nicaragua

Sylvia Mwehozi
2 Januari 2024

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amehimiza mazungumzo ya kumaliza tofauti wakati mapadri zaidi wa kanisa hilo wakizidi kushikiliwa nchini Nicaragua.

Nicaragua| Daniel Ortega
Rais wa Nicaragua Daniel OrtegaPicha: Iranian Presidency/ZUMA Press Wire/picture alliance

Mapadri 14 wa Nikaragua wametiwa mbaroni katika msako mkali dhidi ya Kanisa Katoliki katika nchi hiyo ya Amerika ya Kati na kumfanya Papa Francis kutoa wito wa mazungumzo wakati wa sala yake ya Jumatatu.

Kulingana na orodha iliyoandaliwa na mtaalamu anayeshughulikia masuala ya kanisa la Nikaragua ambaye anaishi uhamishoni nchini Marekani Martha Molina, Padri mwingine anayeitwa Gustavo Sandino kutoka eneo la kaskazini la Jinotega alikamatwa usiku wa mkesha wa mwaka mpya.

Baadhi ya wafungwa wa kisiasa wa Nicaragua walioachiwa kutoka jela mapema mwaka jana. Picha: Lynne Sladky/AP/picture alliance

Kukamatwa kwake ni tukio la hivi karibuni zaidi katika wimbi la kamata kamati chini ya Rais wa mrengo wa kushoto anayeongoza kwa mkono wa chuma Daniel Ortega, ambalo lilianza Desemba 20 kwa kumkamata Askofu Isidoro Mora.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis alisema kuwa anafuatilia kwa ukaribu kinachoendelea Nicaragua, ambako maaskofu na mapadri wamenyimwa uhuru wao. Francis amehimiza mazungumzo kama njia ya kutatua changamoto.

Uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na serikali ya Ortega ulidorora wakati wa maandamano ya kupinga mageuzi ya mafao ya kijamii mwaka 2018, ambayo Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa yalisababisha vifo vya takriban watu 300.

Ortega analituhumu kanisa kwa kuunga mkono upinzani wakati wa maandamano hayo, baada ya kanisa kuwahifadhi waandamanaji.

Maandamano hayo yalianza kutokana na kile ambacho wanaharakati wa haki za binadamu wanaona kama ni ukandamizaji mkali wa mtu yeyote anayechukuliwa kuwa mkosoaji wa serikali.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Andrew Medichini/AP photo/picture alliance

Ortega ni kiongozi wa zamani wa wapiganaji wa msituni ambaye alisaidia kuongoza mapinduzi ambayo yalipindua utawala wa mrengo wa kulia unaoungwa mkono na Marekani mwaka 1979. Kisha alitawala nchi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Soma kuhusu: Nicaragua yawachia huru wapinzani 222 na kuwapeleka Marekani

Alirejea madarakani mwaka 2007, na amekuwa akishutumiwa kwa ubabe huku akiwafukuza na kuwafunga wapinzani, kufuta ukomo wa mihula ya urais na kutwaa udhibiti wa mihimi yote ya serikali. Taifa hilo la Amerika ya Kati limefunga zaidi ya mashirika 3,000, asasi za kiraia na vyama vya wafanyikazi kufuatia maandamano ya 2018.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW