1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Papa Francis ahitimisha ziara katika nchi za Asia-Pasifiki

13 Septemba 2024

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis leo hii amehitimisha ziara yake ndefu zaidi kwenye mataifa manne ya Asia-Pasifiki, safari ya jumla ya kilometa 32,000 na iliyokuwa na changamoto nyingi.

Singapore | Papa Francis akiwasalimia watu
Papa Francis akiwasalimia watu huko SingaporePicha: Vincent Thian/AP Photo/picture alliance

Ziara hiyo iliyoanza Septemba 2 hadi 13, ilimfikisha Papa Francis katika mataifa mawili maskini zaidi duniani ya Papua New Guinea na Timor Mashariki ambalo pia ni taifa lenye asilimia kubwa ya waumini wa Kanisa Katoliki nje ya Vatican.

Papa Francis mwenye umri wa mika 87, alitembelea pia moja kati ya mataifa tajiri zaidi duniani ya Singapore pamoja na taifa lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu la Indonesia na lenye jumla ya watu milioni  242.

Soma pia: Papa, Imamu wa Indonesia waonya dhidi ya uchochezi wa kidini

Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kusisitiza umuhimu wa eneo hilo kwa Kanisa Katoliki, ikiwa ni moja wapo ya maeneo machache duniani yanayoshuhudia ukuaji wa ushawishi wa Kanisa hilo hasa kwa kuzingatia idadi ya waumini wanaobatizwa.

Ziara ya Papa Francis  ilipokelewa kwa shauku kubwa na kuukusanya umati mkubwa wa watu Picha: Gregorio Borgia/AP/dpa/picture alliance

Ziara ya Papa Francis  ilipokelewa kwa shauku kubwa na kuukusanya umati mkubwa wa watu katika mataifa yote aliyoyatembelea. Nchini Indonesia na Papua New Guinea Papa Francis aliongoza misa mbele ya watu 100,000, wengine zaidi ya 50,000 walimlaki huko Singapore huku jumla ya waumini 600,000 wakishiriki maombi nchini Timor Mashariki ikiwa ni karibu nusu ya idadi jumla ya watu wa nchi hiyo.

Soma pia: Papa Francis awasili Singapore na kulakiwa na maelfu

Kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani alitumia safari hiyo ili kuangazia baadhi ya vipaumbele vyake muhimu ikiwa ni pamoja na masuala ya kidini na kitamaduni, kutunza mazingira na kusisitiza kuhusu mambo ya kiroho pamoja na maendeleo ya kiuchumi.

Miito iliyotolewa na Papa Francis kwenye ziara yake

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa FrancisPicha: Dita Alangkara/AP/dpa/picture alliance

Nchini Indonesia, Papa Francis aliitaka nchi hiyo kutimiza ahadi yake ya kuheshimu tofauti za kidini na kupiga vita vitendo vya kutovumiliana. Pia alifanya mikutano na Rais anayemaliza muda wake Joko Widodo pamoja na Rais mteule Prabowo Subianto.

Soma pia: Waumini 600,000 chini Timor Mashariki washirika ibada ya misa iliyoongozwa na Papa Francis

Huko Papua New Guinea, Papa Francis alisafiri hadi katika jiji la mbali la Vanimo lililopo kwenye msitu wa kaskazini-magharibi ambapo alipeleka msaada wa tani za dawa, nguo na vifaa vingine. Alipokelewa na watu wapatao 20,000 waliokuwa wakiimba na kucheza huku akiwatolea wito wa umoja na kuepukana na mizozo ya kikabila eneo hilo.

Kwa ujumla, Papa Francis alihitimisha ziara yake kwa ujumbe wa uvumilivu akiwataka watu wenye imani tofauti kushiriki katika mazungumzo yenye nia ya kujenga badala ya kuwa na misimo mikali. Papa Francis alisema kuwa dini zote ni njia ya kumfikia Mungu na zinatumiwa tu kwa lugha tofauti kumfikia Yeye na kusisitiza kuwa Mungu ni wa wote.

(Chanzo: AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW