1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Papa aionya Mongolia kuhusu rushwa na uharibifu wa mazingira

Angela Mdungu
2 Septemba 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesifu busara za watu wa Mongolia kwa kudumisha amani na ustahimilivu wa kidini huku akiitahadharisha nchi hiyo juu ya rushwa pamoja na uharibifu wa mazingira.

Papa Francis akiwa ziarani Mongolia
Papa Francis akiwa ziarani MongoliaPicha: Vatican Media/Reuters

Papa Francis mwenye miaka 86, ameyasema hayo katika ziara yake ya siku tatu nchini Mongolia iliyoanza siku ya Ijumaa ambapo amekaribishwa kwa sherehe rasmi iliyokuwa na gwaride la wapanda farasi mbele ya Kasri la serikali.

Amekutana na Rais wa Mongolia, Ukhnaagiin Khurelsukh, na kutia saini kitabu cha wageni ambapo ameandika kuwa, "anatembelea taifa changa lenye historia kongwe, la kisasa na lenye utajiri wa tamaduni."

Papa Francis, ameitembelea nchi hiyo yenye idadi ndogo zaidi ya waumini wa dhehebu la Kikatoliki. Mongolia ina Wakatoliki 1,450. Awali aliusalimu umati wa watu waliokuwa wamesimama mbele ya sanamu la shaba la Gengis Khan huku vijana wa kikatoliki wakimshangilia. Safari hiyo pia imewavuta waumini wa Kikatoliki wa China ambao walihudhuria pia hafla ya kumkaribisha Papa.

Ziara hiyo ya kidiplomasia ya Papa Francis inalenga kutafuta mshirika asiye na upande wowote, wakati Vatican ikifanya juhudi za kuimarisha uhusiano wake na Mongolia pamoja na mataifa jirani.

Awasifu Washamani na waumini wa Buddha kwa kuishi kwa amani na mazingira

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema, utamaduni wa Washamani na waumini wa Buddha wa kuishi kwa amani na mazingira pamoja na viumbe vilivyomo ndani yake kunaweza kuchangia pakubwa juhudi za kuinusuru na kuihifadhi sayari ya dunia.

Papa Francis (kushoto) akiwa na Rais wa Mongolia, Ukhnaagin Khurelsukh (kulia)Picha: Andrew Medichini/AP/picture alliance

Pamoja na Papa Francis kuipongeza pia Mongolia kwa ustahimilivu wa kidini, na kwa kutokuwa na sera za uundaji wa silaha za nyuklia amesema pia kuwa, dini inaweza kusaidia kujilinda dhidi ya kitisho cha rushwa ambayo ni kikwazo kwa maendeleo ya jamii yoyote ya binaadamu. Ameongeza kuwa, serikali hazina sababu ya kulihofia kanisa katoliki kwani halina ajenda yoyote ya kisiasa.

Soma zaidi:China yatuma Ujumbe kwa Vatican baada ya Papa Francis kuzuru Mongolia

Mongolia imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya ufisadi na uharibifu wa mazingira katika miaka ya hivi karibuni. Mji wake mkuu Ulaanbaatar ni moja kati ya miji yenye kiwango kibaya zaidi cha hali ya hewa. Maafisa wake wamekuwa wakituhumiwa kwa rushwa hali iliyosababisha kuzuka kwa maandamano mwaka uliopita.

Sehemu kubwa ya nchi hiyo pia iko hatarini kuwa jangwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, uchimbaji madini na kulisha mifugo mingi kupita kiasi katika baadhi ya maeneo. Ziara ya Papa Francis inadhamiria pia kupeleka ujumbe wa kanisa kwa maeneo ya mbali na  yasiyopewa kipaumbele.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW