1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi makali Gaza, Papa atoa wito

11 Oktoba 2023

Jeshi la Israel limefanya mashambulizi ya ndege usiku kucha katika viunga vya ukanda wa Gaza, huku vita vyake dhidi ya kundi la Hamas vilkiingia siku ya tano Jumatano. Zaidi ya watu 2,200 wameuawa katika vita hivyo.

Ukanda wa Gaza| Mashambulizi wa anga
Moto ukiripuka kutokana na shambulizi la ndege la Israel mjini Gaza. Idadi ya vifo huko Gaza imefikia 1,055, huko Israel ikiripoti vifo 1,200.Picha: MOHAMMED ABED/AFP

Vita hivyo vya Israel dhidi ya Hamas, ambavyo tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,200 kwa pande zote, vinatarajiwa kuongezeka.

Shambulio la mwishoni mwa wiki, ambalo Hamas ilisema lilikuwa kisasi kutokana na hali inayozidi kuwa mbaya kwa Wapalestina walioko chini ya ukaliaji wa Israel, limechochea azma ya Israel kuvunja udhibiti wa kundi hilo katika ukanda wa Gaza.

Hamas inatambuliwa na Marekani, Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani, na mataifa mengine kuwa ni kundi la kigaidi.

Jeshi la Israel limesema zaidi ya watu 1,200, wakiwemo wanajeshi wasiopungua 169, wamekufa nchini Israel tangu uvamizi wa siku ya Jumamosi.

Soma pia: Israel inaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya ukanda wa Gaza

Mjini Gaza, wizara ya afya imesema watu karibu 1055 wameuawa na wengine 5,000 wamejeruhiwa. Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi wa Palestina, UNRWA, linasema watu 250,000 wamepoteza makazi yao Gaza.

MAshambulizi ya Israel yamesambaratisha vijiji vizima na kuvifanya visivyokalika tena.Picha: BELAL AL SABBAGH/AFP

Papa aihimiza Hamas kuwaachia mateka, aelezea wasiwasi kuhusu mzingiro Gaza

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, katika matamshi yake makali tangu kuanza kwa mzozo huo, alitoa wito siku ya Jumatano wa kuachiliwa kwa mateka wote waliochukuliwa na wanamgambo wa Hamas na kusema Israel ina haki ya kujilinda.

Akizungumza mwishoni mwa hadhara yake ya kila wiki kwa maelfu ya watu katika uwanja wa St. Peter, pia alielezea wasiwasi wake juu ya mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza.

"Ninaendelea kufuatilia, kwa uchungu na wasiwasi, kile kinachotokea Israel na Palestina. Watu wengi sana waliuawa, na wengine kujeruhiwa. Naziombea familia zilizoshuhudia siku ya sikukuu ikigeuka kuwa siku ya maombolezo, na ninaomba kwamba mateka waachiliwe mara moja," alisema.

Soma pia: Umoja wa Mataifa waionya Israel juu ya kuizingira Hamas

"Ni haki ya wale wanaoshambuliwa kujilinda, lakini nina wasiwasi mkubwa na mzingiro mzima wa Wapalestina wanaoishi Gaza, ambako pia kumekuwa na wahasiriwa wengi wasio na hatia," alisema.

Erdogan: Israel haitendi kama taifa Gaza

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekosoa mwenendo wa Israel Gaza, akisema Jumatano kwamba haitendi "kama taifa."

"Israeli isisahau kwamba ikiwa itafanya kama shirika badala ya serikali, itamaliza kwa kutendewa hivyo," amesema Erdgoan akikosoa "mbinu za aibu" za jeshi la Israeli.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, ameitaka Hamas kuwaachia mateka na kuelezea wasiwasi kuhusu mzingiro jumla wa Gaza.Picha: Yara Nardi/REUTERS

Israel iliikatia Gaza ugavi wa chakula, mafuta, umeme na dawa, na kivuko pekee kilichosalia kutokea Misri kilifungwa jana Jumanne baada ya mashambulizi ya ndege kupiga karibu na kivuko hicho.

Mamlaka ya Umeme ya Gaza imesema mtambo wake wa kufua umeme utaishiwa mafuta ndani ya masaa machache, na kuliacha eneo hilo bila huduma ya umeme.

Mkuu wa shirika la misaada la Madaktari wasio na Mipaka anaesimamia maeneo ya Wapalestina, amesema ana wasiwasi pia kwamba timu ya madaktari wa shirika hilo mjini Gaza wataishiwa ugavi wa dawa muda si mrefu.

Je, huu ndiyo mwisho wa Hamas?

Israel inachukuwa mwekeleo mpya kwa vita vyake vya angani, ikiwaonya raia kuondoka eneo moja baada ya jengine na kisha kufanya mashambulizi makali. Pia imewakusanya wanajeshi wa akiba 360,000.

Soma pia: Israel yasema wanamgambo 1,500 wa Hamas wameuwawa Gaza

Mbinu hizi mpya zinaashiria lengo jipya. Duru nne za mwisho za mapigano ya Israel na Hamas kati ya 2008 na 2021 zilimalizika pasina mshindi wa wazi, ambapo Hamas ilidhoofishwa lakini ikasalia na udhibiti wa ukanda huo.

Israel kuuzingira Ukanda wa Gaza

02:48

This browser does not support the video element.

Safari hii serikali ya Israel iko chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa umma kuiondoa Hamas, lengo ambalo huko nyuma lilizingatiwa kutowezekana kwa sababu hilo lingehitaji kuukalia tena ukanda wa Gaza, alau kwa muda. 

Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav amesema siku ya Jumanne kuwa ameondoa vizuwizi vyote safari hii, na kuongeza kuwa watamuondoa yeyote anaepigana nao, na kutumia kila zana walionayo.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW