1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis alaani mashambulizi barani Afrika

25 Desemba 2019

Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, ametumia hotuba yake ya Krismasi kukemea matukio ya kigaidi na siasa kali magharibi mwa Afrika, ikiwa ni siku moja baada ya wanamgambo kuwauwa watu 35 nchini Burkina Faso.

Weihnachten Christentum l Urbi et orbi - Weihnachtssegen des Papsts, Vatikan
Picha: AFP/A. Pizzoli

Akitowa ujumbe wake mjini Vatican hivi leo (Jumatano, Dis. 25), Papa Francis amelaani mashambulizi dhidi ya Wakristo barani Afrika na amewaombea wahanga wa mizozo, majanga ya kimaumbile na maradhi kwenye bara hilo.

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki ametoa wito wa kufarijiwa "wale wanaoadhibiwa kwa ajili ya imani zao za kidini, hasa wamishionari na waumini waliotekwa, na wahanga wa mashambulizi ya makundi ya itikadi kali, hasa nchini Burkina Faso, Mali, Niger na Nigeria."

Kauli ya Papa Francis inakuja wakati kukiwa na ripoti kwamba wanamgambo wa itikadi kali nchini Burkina Faso wamewauwa watu 35, wengi wao wanawake, baada ya kushambulia maeneo mawili tofauti kwa wakati mmoja kwenye mji mmoja wa kaskazini mwa nchi hiyo na kambi ya kijeshi.

Katika hotuba yake ya Krismasi, mbali na kutaja matukio ya kigaidi barani Afrika, Papa Francis aliwaombea pia wale wanaoteseka kutokana na ghasia, majanga ya kimaumbile au mripuko wa maradhi, na pia wahamiaji wanaojaribu kuvuka bahari kuingia barani Ulaya kusaka maisha bora.

"Ni dhuluma ndiyo inayowafanya wavuke majangwa na bahari ambazo huwa makaburi yao," alisema kwenye ujumbe wake wa "Urbi et Orbi" (Kwa Mji na kwa Ulimwengu) katika makao makuu ya kanisa hilo, Vatican.

Mashambulizi ya jana nchini Burkina Faso yanatajwa kuwa mashambulizi mabaya kabisa kuwahi kufanywa katika taifa hilo la magharibi mwa Afrika, ambalo limekuwa likishuhudia mashambulizi ya makundi ya kigaidi kwa kipindi kirefu sasa.

Wanamgambo 80 wauawa

Jeshi likiwa kwenye operesheni dhidi ya magaidi nchini Burkina Faso.Picha: picture-alliance/dpa/A. Yempapou

Wanajeshi saba wa serikali na wanamgambo 80 waliuawa pia wakati wakiwa kwenye mapambano katika mji wa Arbinda, jimbo la Soum, ambayo yalichukuwa masaa kadhaa, kwa mujibu wa jeshi.

"Kundi kubwa la magaidi lilivamia kambi ya kijeshi na raia kwenye mji wa Arbinda," ilisema taarifa ya mkuu wa majeshi.

"Mashambulizi ya kikatili yalisababisha vifo vya watu 35, wengi wao wakiwa wanawake," alisema Rais Roch Marc Christian Kabore kupitia mtandao wa Twitter, ambako pia aliwapongeza wanajeshi kwa ushujaa na kujitolea kwao.

Waziri wa mawasiliano na msemaji wa serikali, Remis Dandjinou, alisema kwamba miongoni mwa raia waliouawa, 31 walikuwa wanawake, akiongeza kwamba wanajeshi 20 na raia sita walijeruhiwa. 

Rais Kabore alitangaza kipindi cha masaa 48 ya maombolezo ya kitaifa.

Ripoti zinasema kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na wapiganaji waliowasili wakiwa wamepanda pikipiki na yalichukuwa masaa kadhaa kabla ya jeshi likisaidiwa na kikosi cha anga hawajawarejesha nyuma. 

Hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo, lakini mashambulizi ya kigaidi kama hayo yamekuwa kila mara yakihusishwa na wanamgambo wenye mahusiano na Al-Qaida na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, IS.