1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVatican

Papa Francis alaani ''uhalifu wa kivita '' dhidi ya raia

8 Januari 2024

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amelaani "uhalifu wa kivita" unaofanywa dhidi ya raia katika mizozo kama ile inayoendelea katika Ukanda wa Gaza na nchini Ukraine

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis akiwa mjini Vatica mnamo Juni 7, 2023
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Ettore Ferrari/ANSA/picture alliance

Katika hotuba yake ya mwaka mpya kwa wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao katika makao makuu ya kanisa katoliki mjini Vatican,  Papa Francis amezungumzia masuala mbali mbali yanayoathiri ubinadamu na kuongezeka kwa ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu inayoruhusu kufanyika kwa maovu hayo.

Masuala yalioangaziwa na Papa Francis

Papa, amezungumzia kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine, vita vya Israel katika ukanda waGaza, mizozo ya uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi pamoja na utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Soma pia. Papa Francis afadhaishwa na kurejea kwa mapigano Ukanda wa Gaza

Kuhusu vita, kiongozi huyo wa kanisa Katoliki, amesema, tofauti kati ya malengo ya kijeshi na kiraia haziheshimiwi tena. Ameongeza kuwa hakuna mzozo ambao hauishii kwa namna fulani kuwalenga raia bila kubagua na kwamba mapigano nchini Ukraine na katika Ukanda wa Gaza ni ushahidi wa hali hiyo.

Hotuba ya Papa yasheheni miito ya kusitishwa kwa mapigano

Katika hotuba hiyo iliyosheheni miito ya kusitishwa kwa mapigano kote ulimwenguni, Papa amesema, watu hawapaswi kusahau kwamba ''ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu ni uhalifu wa kivita".

Papa ameongeza kuwa anatumaini jamii ya kimataifa itafuatilia kwa dhamira suluhu la mataifa mawili, moja la Israel na moja la Palestina, pamoja na hadhi maalum iliyohakikishwa kimataifa kwa ajili ya mji wa Jerusalem, ili hatimaye Waisraeli na Wapalestina waishi kwa amani na usalama.

Juhudi za uokoaji kutokana na shambulizi la Israel zaendelezwa katika ukanda wa GazaPicha: Khaled Omar/Xinhua/picture alliance

Kwa mara nyingine tena, Papa Francis amelaani shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na wanamgambo wa Hamas, ambalo lilisababisha takriban vifo 1,140 nchini Israel, wengi wao wakiwa raia, hii ikiwa kulingana na takwimu rasmi za Israeli.

Papa alaani mtindo wa wanawake kubebeana mimba kwa malipo

Kuhusu suala la mtindo wa wanawake kubebeana mimba kwa malipo, Papa Francis amesema kuwa maisha ya mtoto ambaye hajazaliwa lazima yalindwe na sio "kukandamizwa au kugeuzwa kuwa bidhaa ya biashara haramu."

Soma pia:Papa Francis airai Hamas kuwaachia mateka, aeleza wasiwas mzingiro Gaza

Kiongozi huyo wa Kiroho wa kanisa katoliki duniani anautazama  mpango wa mwanamke kubeba mimba kwa niaba ya mwingine kwa malipo, kama kitendo cha dharau kinachosimamia ukiukwaji mkubwa wa utu wa mwanamke husika na mtoto, kwa kuzingatia matumizi mabaya ya hali ya mahitaji ya mwanamke husika.

Soma piaPapa Francis ahimiza mazungumzo wakati mapadri zaidi wakikamatwa Nicaragua

Hotuba ya papa pia imeangazia majanga mbalimbali ya kibinadamu na wakimbizi barani Afrika, na bila kutaja majina kulaani mapinduzi ya kijeshi na chaguzi katika mataifa kadhaa ya kiafrika zilizokabiliwa na madai ya "rushwa, vitisho na vurugu."

Wakati huo huo,Papaametoa wito wa mazungumzo ya kidiplomasia yenye heshima na serikali ya Nicaragua kutatua kile alichokiita "mgogoro wa muda mrefu."

Serikali ya Nicaragua yalishtumu kanisa Katoliki kwa kusaidia maandamano dhidi yake

Ukandamizaji wa serikali ya nchi hiyo dhidi ya Kanisa Katoliki umesababisha kuwekwa kizuizini kwa mamia ya mapadre na maaskofu. Serikali hiyo imelishtumu kanisa Katoliki kwa kusaidia maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wake, hali inayoonekana kama jaribio la mapinduzi.

Papa Francis pia ametoa wito wa kurejelewa kwa mazungumzo ya nyuklia ya Iran kuhakikisha usalama wa baadaye kwa wote.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW