1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aliidhinisha mpango wa siri kumwokoa Mtawa

Sylvia Mwehozi
6 Mei 2022

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametajwa kuidhinisha operesheni ya siri ya kiasi cha euro milioni moja kwa ajili ya kumkomboa Mtawa wa Colombia aliyekuwa ametekwa na wanamgambo wa itikadi kali Mali.

Kardinal Angelo Becciu und Papst Franziskus
Picha: Stefano Spaziani/picture alliance

Hayo yamebainika katika ushahidi uliotolewa na Kadinali Angelo Becciu mbele ya mahakama mjini Vatican siku ya Alhamis. Becciu mwenye umri wa miaka 73, ni Kadinali pekee miongoni mwa washitakiwa wengine 10 katika kesi ya ubadhirifu wa fedha iliyoanza mwezi Julai mwaka uliopita. Pia ameileza mahakama kwamba hakuwa na mahusiano yasiyofaa na mwanamke wa Kiitaliano ambaye alikuwa kama mpatanishi katika operesheni ya kumkomboa Mtawa huyo.

Mtawa huyo anayeitwa Gloria Cecilia Narvaez wa Colombia, alitekwa na wanamgambo wa kundi la Macina Liberation Front ambao wana mafungamano na kundi la Al-Qaeda nchini Mali mnamo mwaka 2017. Kadinali Becciu ametoa ushuhuda kwamba Cecilia Marogna ambaye pia ni mshitakiwa ndiye aliyemuunganisha na kampuni ya Uingereza ya usalama mwaka 2018 ili kumwokoa mtawa.

Anadai kuwa alimueleza Papa Francis juu ya operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa "mtandao wa mawasiliano" na fedha ya kumkomboa mtawa, vyote vingegharimu takribani euro milioni moja. "Aliidhinisha. Ninaweza kusema kwamba kila hatua ya operesheni hiyo ilikuwa imeidhinishwa na Baba Mtakatifu", alisema Becciu katika ushahidi wake.Papa Francis aondoa usiri juu ya kashfa za udhalilishaji wa kingono

Becciu ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa serikali kuu ya Vatican kati ya mwaka 2011-2018, anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha, matumizi mabaya ya ofisi na kushawishi shahidi wa uongo. Amekana mashitaka yote.

Mtawa Gloria Cecilia Narvaez Picha: Leonardo Muñoz/AP/picture alliance

Kwenye ushahidi wake Kadinali huyo amebainisha kwamba akaunti maalum ya operesheni hiyo iliundwa na Sekretarieti ya serikali ya Vatican na kwamba malipo yalifanyika katika akaunti zilizotolewa na Marogna. Ameongeza kuwa kampuni iliyokodiwa ya ujasusi ilianzisha mawasiliano na watekaji lakini hakusema ikiwa malipo ya kikomboleo yalifanyika. Kulingana na ushahidi wake, mipango yote hiyo ilibaki kuwa siri dhidi ya mkuu wa usalama wa Vatican kwa wakati huo kwasababu uvujaji wowote wa taarifa ungeweza kuibua ukosoaji wa kimataifa na "kuhatarisha maisha na usalama wa Wamishionari wengine".

Papa alimfuta kazi Kadinali Becciukutoka nafasi nyingine mjini Vatican mwaka wa 2020,zikanusha. Miezi miwili iliyopita, Papa aliondoa kiapo cha Becciu cha "Usiri wa Papa" ili aweze kujibu maswali yanayohusiana na Marogna na kutekwa nyara kwa mtawa.

Kesi hiyo inahusu zaidi ununuzi wa jengo katika eneo la kifahari jijini London kama uwekezaji uliogharimu takriban euro milioni 350 kuanzia mwaka 2014. Lakini mpango huo ulikwenda mrama na Vatican ilipoteza karibu euro milioni 217.

Katika kesi hiyo iliyosikilizwa karibu saa saba, mwendesha mashtaka wa Vatican Alessandro Diddi alimbana Kadinali Becciu kuhusu vipengele vingine vya mkataba huo, uhusiano wa kitaasisi wa Kadinali na maafisa wengine wa Vatican sambamba na benki ambazo zilitumika.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na viongozi na watumishi wa zamani wa Vatican ambao wanashtakiwa kwa ubadhirifu na uhalifu mwingine wa kifedha unaohusishwa na mkataba wa mali isiyohamishika.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW