1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis amewasili Kenya

25 Novemba 2015

Papa Francis amewasili Kenya katika ziara yake ya kwanza ya kihistoria barani Afrika bara linalokabiliwa na changamoto za kiusalama. Mamilioni wanatarajiwa kuhudhuria misa Nairobi.

Papst Franziskus in Florenz
Picha: Reuters/S. Rellandini

Papa Francis ameondoka nchini Roma Italia leo kuelekea Kenya kwa ziara yake ya kwanza ya kihistoria barani Afrika bara ambalo linakabiliwa na changamoto za kiusalama na ya tano katika maeneo tafauti ya dunia tangu akamate wadhifa huo.

Papa huyo mwenye umri wa miaka 78 ni wa tatu kuzuru bara hilo,pia amepangiwa kutembelea Uganda na Jamhuri ya Afrika ya kati inayokumbwa na vita kwa ziara ya siku sita.

Katika mitaa ya jiji kuu la Kenya Nairobi ambako kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni anatarajiwa kuwasili mwendo wa saa kumi na moja jioni, huku mabango makubwa yametundikwa kumkaribisha.

Umati wa watu unatarajiwa kujitokeza kulaki msafara wake.Gazeti la the Standard nchini Kenya liliandika kichwa "Karibu Papa Francis" kumkaribisha huku ujumbe huo ukirudiwa kwa lugha ya kilatini Grata Franciscus Pontifex.

Ufisadi kuangaziwa

Papa Francis atalakiwa nchini Kenya na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. Katika Ikulu ya Nairobi atakako kuwa na mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta, Papa Francis anatarajiwa kugusia swala la Ufisadi na tofauti iliyopo kati ya masikini na tajiri, maswala ambayo ni muhimu kwa wakenya.

Kiongozi huyo ataongoza misa itakayohudhuriwa watu karibu 500,000 siku ya Alhamisi. Nchini Uganda miongoni mwa mengine atazuru mahala walikozikwa viongozi wa kikristo waliouliwa nchini humo. Papa Francis anatarajiwa kutumia gari rasmi lililo wazi ambalo hulitumia anapofanya ziara .

Ziara katika Jamhuri ya Afrika itafanyika kama ilivyopangwa licha ya maonyo kadhaa kutoka kwa wanajeshi wa kusimamia amani amani wa Ufaransa nchini humo kuwa hawawezi kumhakikishia Papa Francis usalama.

Maafisa wa Vatikan wamesema mabadiliko ya dakika za mwisho mwisho ya utaratibu wa ziara ya Papa Francis yatafanyika tu ikiwa atajulishwa kitisho halisi kitakachohatarisha maisha ya maelfu ya waumini wanaotarajiwa kushuhudia ziara hiyo ya Papa huku wengi wao wakitarajiwa kusafiri kutoka mbali maeneo ya mbali na kutoka mataifa jirani.

Wanajeshi wa ufaransa wakisimama Karibu na vifaru vya kijeshiPicha: P. Pabandji/AFP/Getty Images

Jamhuri ya Afrika ya kati ambako atafungua mlango mtakatifu katika Kanisa kuu mjini Bangui , siku 10 kabla ya kuadhimisha sherehe kuu za kanisa Katoliki kwa wito wa kusameheyana na maridhiano. Atauzuru pia msikiti wa Bangui na kambi ya wakimbizi.

Kuna uwezekano wa kupunguza ratiba ya ziara

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya ya kati Catherine Samba-Panza ameshiria juu ya uwezekano wa kupunguzwa ratiba ya ziara ya Papa kwa zingatio la hali ya usalama na shughuli zote kufanyika katika uwanja wa ndege wa bangui ,eneo ambalo wanajeshi wa Ufaransa wanasema kuwa na uhakika wa kutoa ulinzi kwa kiongozi huyo wa wakatoliki bilioni 1.2 duniani. Afrika ina waumini milioni 180,000 na idadi hiyo inaendelea kuongezeka.

Mwandishi: Bernard Maranga/AFP/DPA.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman