1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aomba msamaha nchini Chile

Isaac Gamba
17 Januari 2018

Papa Francis katika siku yake ya kwanza ya ziara ya wiki moja katika mataifa ya Amerika ya Kusini ameomba msamaha kutokana na madhara yaliyosababishwa na udhalilishaji kingono nchini Chile.

Chile Papst Franziskus in Santiago | Messe O'Higgins Park
Picha: Getty Images/AFP/P.P. Brune

 Matamshi ya Papa Francis yanakuja mnamo wakati idadi ya makanisa ya kikatoliki yaliyoshambuliwa katika kipindi cha wiki iliyopita  kupinga ziara yake nchini nchini Chile ikifikia makanisa manane ikiwa ni pamoja na kanisa moja lililochomwa moto katika mkoa wa Auricania ambako  Papa Francis aliendesha misa.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji mbele ya eneo ambalo Papa Francis alikuwa akiongoza misa katika mji wa Santiago wakipinga ziara ya Papa nchini humo.

Licha ya matukio hayo idadi kubwa ya wananchi wa Chile walijitokeza kumuona Papa Francis katika ziara yake ya kwanza nchini humo ikiwa ni pamoja na watu wanaokadiriwa kufikia 400,000 waliojitokeza katika misa aliyoiongoza.

Taarifa iliyotolewa na makao makuu ya kanisa Katoliki mjini Vatican inasema Papa Francis alikutana na kundi dogo la wahanga waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kingono mjini Chile ambapo alitumia nafasi hiyo kuomba pamoja nao na kushuhudiwa akibubujikwa pia na machozi.

Aidha Papa Francis alisababisha baadhi ya wafungwa kububujikwa machozi alipotembelea gereza la wanawake nchini humo.

Hata hivyo matamshi yake aliyoyatoa katika hotuba yake ya kwanza yalikuwa ni yale ambayo wachile wengi walikuwa wakitarajia kuyasikia .

 

Aonesha masikitiko yake kwa udhalilishaji huo

Akizungumza  katika makazi ya rais , Papa Francias alimueleza rais wa Chile Michelle Bachelet, wabunge, majaji na maafisa wengine kuwa anajisikia kuwa mwenye aibu na anaelezea masikitiko yake kutokana na vitendo vya udhalilishaji kingono dhidi ya watoto  vilivyofanywa  na viongozi wa kidini nchini Chile.

Rais wa Chile, Michelle BacheletPicha: Reuters/M. Brindicci

Papa Francis alisema  yeye ni miongoni mwa maaskofu wa kanisa katoliki wanaoona ni muhimu kuomba radhi na kufanya kila juhudi kuwasaidia wahanga  ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa matukio ya aina hiyo hayajirudii tena.

 

 Papa Francis hakutolea mfano wa padri mmoja,  Fernando Karidima  ambaye mwaka 2011 alifungiwa na makao makuu ya kanisa hilo mjini Vatican  kujishughulisha na shughuli zote za huduma ya kichungaji kutokana na tuhuma za kuwadhalilisha watoto kingono na pia hakumtolea mfano askofu wa mjini Santiago anayedaiwa kukiri kuwa na taarifa kuhusiana na malalamiko yaliyotolewa dhidi ya Karadima lakini akashindwa kuchukua hatua dhidi yake.

Karadima ambaye alijijengea heshima kubwa kutokana na mafanikio yake ya kuwezesha kuibua maaasikofu kadhaa anakabiliwa na kashifa kufuatia  malalamiko yaliyotolewa dhidi yake na baadhi ya wahanga wa vitendo vya udhalilishaji kijinsia wakidai  kuwa aliwabusu na kuwadhalilisha kijinsia wakati walipokuwa vijana.

Papa Francis alisema vitendo hivyo vya udhalilishaji si tu kwamba vimesababisha majeraha yasiyotibika kwa wahanga wa matukio hayo bali pia vimeharibu heshima katika jamiii ya waumini wa kanisa hilo na kwa mtu yeyote anayetoa huduma ya kichungaji.

Anne Barret ambaye anatoka katika shirika linalofuatilia mienendo ya maaasikofu alimsifu Papa Francis kwa kuanza hotuba yake kwa kuomba msamaha lakini akaongeza kuwa wananachi wa Chile wanamtarajia achukue hatua dhidi ya viongozi wasiokuwa na maadili ndani ya kanisa hilo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ape/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga