Papa aomba msamaha kwa niaba ya Kanisa Katoliki
14 Oktoba 2015Papa Francis ameuomba msamaha huo alipokuwa akizungumza leo mchana wakati akiwahubiria maelfu ya watu waliokusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Peter, mjini Vatican, katika utaratibu wake wa kila juma.
''Kabla ya kuanza kwa Katekesi, nataka kwa niaba ya Kanisa, kuomba msamaha kwa kashfa ambazo hivi karibuni zimeikumba Roma na Vatican. Naomba msamaha wenu,'' alisema Papa Francis.
Msamaha huo ameuomba katika kipindi ambacho Kanisa Katoliki limejikuta kwenye kashfa kadhaa, ikiwemo ile ya kujitokeza hadharani kwa Padri shoga anayepinga msimamo wa kanisa kuhusu mapenzi ya jinsia moja na kauli dhidi ya Meya wa Roma, aliyejiuzulu wiki iliyopita.
Papa Francis ameomba radhi wakati anaongoza mkutano wa wiki tatu wa baraza la makardinali na maaskofu kujadili namna ya kupitia mafundisho ya kanisa hilo pamoja na kuhusu masuala ya familia.
Hata hivyo, Papa hakutaja hasa aina ya kashfa anayoizungumzia wala kutoa mifano. Siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo kuhusu masuala ya familia, padri wa Poland alitangaza hadharani kuwa yeye ni shoga, huku mpenzi wake akiwa pembeni yake. Padri huyo aliyefanya kazi yake Vatican kwa miaka 17, alifukuzwa kazi yake ya ukasisi.
Kashfa zaongozana
Kashfa hiyo ilifuatiwa na ile ya kujiuzulu kwa Meya wa Roma, Ignazio Marino, kutokana na kashfa ya kuwaandalia karamu marafiki na familia yake kwa kutumia fedha za jiji. Papa na Kanisa walisema kuwa hawana imani na uwezo wa meya huyo katika kuwashughulikia mamilioni ya mahujaji wakati wa 'Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu', utakaoanza mwezi Disemba mwaka huu.
Aidha, katika kashfa nyingine, barua yenye utata iliyovuja ambayo ilionyesha kwamba makardinali kadhaa wahafidhina wamekosoa namna Sinodi hiyo inavyoendeshwa na kuhoji kuhusu maafikiano yoyote yaliyofikiwa kuhusu ndoa katika Kanisa.
Hata hivyo, msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi, ameshutumu vikali kuhusu barua hiyo iliyoandikwa kwa Papa, lakini aliwakumbusha wahusika kwamba utaratibu wa mkutano unaandaliwa na kazi yao ni kufuata utaratibu huo.
Papa Francis ambaye alichaguliwa Machi mwaka 2013, wakati Kanisa Katoliki linakabiliwa na kashfa, ikiwemo ile ya mapadri kuwanyanyasa watoto kingono, leo pia amekutana na ujumbe wa wachimbaji madini 30 wa Chile, ambao walikwama kwenye mgodi kwa siku 70, miaka mitano iliyopita.
Papa aliwashukuru kutokana na imani waliyonayo kwa Mungu na alisema anajua kila mmoja atakuwa na uwezo wa kuelezea maana ya matumaini.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE, APE, DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman