1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis awaomba radhi jamii ya wenyeji wa asili Canada

26 Julai 2022

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis akiwa ziarani nchini Canada, ameomba msamaha wa kihistoria kutokana na ushiriki wa Kanisa Katoliki katika sera mbaya ya shule za bweni za wenyeji wa asili

BdTD | Kanada
Picha: Patrick T. Fallon/AFP

Katika tukio la kwanza la ziara yake ya wiki nzima aliyoiita "hija ya toba", Papa Francis alitembelea ardhi ya jamii nne za wenyeji wa asili ili kufanya maombi katika makaburi na kisha kuomba msamaha uliosubiriwa kwa muda mrefu. Machifu wanne wa jamii hizo za wenyeji wa asili walimsindikiza papa Francis aliyekuwa katika kiti cha magurudumu kuelekea katika moja ya Shule ya bweni ya Wahindi ya Ermineskin.

Katika shule nyengine ya Edmonton huko Alberta, Papa Francis alisema huku akishangiliwa na familia za manusura wa jamii wenyeji wa sili, kuwa anaomba msamaha kwa unyenyekevu mkubwa, na kuwa shule hizo ilikuwa kosa kubwa ambazo zilienda kinyume na mafundisho ya dini hiyo: 

"Hatua ya kwanza ya hija yangu ya toba kati yenu ni ile ya kuomba tena msamaha, ya kuwaambia tena kwamba ninasikitika sana. Ninaomba msamaha, hasa, kwa namna washiriki wengi wa kanisa na jumuiya za kidini walivyoshirikiana bila kujali katika miradi ya uharibifu wa tamaduni uliokuzwa na serikali za wakati huo."

Kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki amesema uchunguzi zaidi na uponyaji vinahitajika.

Picha: Vatican press office/AFP

Unyanyasaji mkubwa kwa jamii za wenyeji wa asili

Zaidi ya watoto 150,000 wa jamii ya wenyeji wa asili nchini Canada walilazimishwa kuhudhuria shule za Kikristo zilizofadhiliwa na serikali kutoka karne ya 19 hadi miaka ya 1970, katika jitihada za kuwatenga na ushawishi wa tamaduni zao za asili. Lengo kuu ilikuwa kuwalazimisha kuwa Wakristo na kuwaingiza katika jamii iliyotawala wakati huo na ambayo serikali zilizopita za Canada zilichukulia kuwa juu ya zingine.

Mji wa Ottawa umekiri kwamba unyanyasaji wa kimwili na kingono ulikuwa umeenea sana katika shule hizo za kikatoliki, huku wanafunzi wakipigwa kwa kosa tu la kuongea lugha yao ya asili. Urithi huo wa unyanyasaji na kutenganishwa na familia, umetajwa na viongozi wa jamii za wenyeji wa asili kuwa chanzo cha janga la kuongezeka viwango vya ulevi na madawa ya kulevya hasa kwenye maeneo ya hifadhi nchini Canada.

Soma zaidi: Makaburi 751 yagunduliwa nchini Canada karibu na shule ya watoto wa kiasili

Ugunduzi wa mwaka uliyopita wa mamia ya makaburi katika shule hizo nchini Canada na Marekani, ulivutia hisia za kimataifa na kumlazimu Papa Francis kukubali wito wa tume ya ukweli na maridhiano wa kuomba msamaha katika ardhi ya Canada, ambako Kanisa Katoliki liliendesha shule za bweni 66 kati ya 139 kote nchini humo.

Msamaha wa Papa Francis nchini Canada kutokana na makosa ya Kanisa Katoliki dhidi ya jamii za wenyeji wa asili, ulizua hisia mseto miongoni mwa jamii. Wakati Papa Francis akiongea wapo walikuwa wakilia, wengine walipiga makofi au kukaa kimya na kusikiliza maneno yake kwa umakini, lakini wengine walimua kutohudhuria kabisa.

(APE)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW